Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kupitia Idara ya Maendeleo ya Jamii leo tarehe 06 Novemba , 2024 wamefanya semina ya utoaji wa elimu ya mikopo ya asilimia 10 ya Halmashauri kwa wananchi wa Kata ya Bonyokwa katika Ulumbi wa Masia lengo ikiwa ni kutekeleza agizo la Serikali kuhakikisha wananchi wanapata Elimu ya mfumo mpya wa uombaji wa mikopo kwa njia za kibenki,
Akiongea na wananchi wa Kata hiyo, Afisa Maendeleo wa Kata ya Bonyokwa Bi. Regina Ng’ongolo ameeleza kuwa lengo la semina hiyo ni kuwaelekeza wananchi sheria na kanuni za mfumo mpya wa uombaji mikopo ya asilimia 10 yenye lengo la kuwawezesha na kuwasaidia wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kujikwamua kiuchumi na kuongeza mapato katika familia na nchi kiujumla.
Aidha, Bi. Regina ametoa wito kwa wananchi wenye nia moja kuunda vikundi mbalimbali na wajitokeze kuomba mikopo hiyo yenye riba nafuu isiyoumiza Na kwa wale ambao bado hawajarejesha warejeshe kwa wakati ili na wanufaika wengine waweze kupata.
Katika Semina hiyo wananchi walielezwa sifa za mkopaji ikiwa ni pamoja na kuwa na kitambulisho/Namba ya NIDA, wakopaji wanatakiwa wasiwe na ajira rasmi , Andiko la Mradi linaloonyesha malengo na matumizi ya mkopo, mukhtasari wa kikao pamoja na nakala za taarifa za kibenki
Sambamba na hilo, mada mbalimbali ziliwasilishwa pamoja na wananchi hao kufundishwa namna ya kuunda vikundi na kuvisaji ili kuweza kupata mikopo isiyo na riba itakayowaongezea kipato kwakuwa mikopo ya awamu hii imelenga kumfikia kila mnufaika kuanzia wafanya biashara wadogo wadogo pamoja na Mama lishe/Baba lishe na Bodaboda.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Postal Address: S.L.P 20950
Telephone: 0738 378 386
Mobile: 0738 378 386
Email: info@dcc.go.tz
Copyright © 2017 Dar es Salaam City Council . All rights reserved.