Na: Hashim Jumbe
BARAZA la Madiwani Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, leo tarehe 09 Machi, 2021 limefanya kikao maalum cha mapitio ya Bajeti ya mwaka 2020/2021 na mapendekezo ya Mpango na Bajeti ya mwaka wa fedha 2021/2022 wenye Jumla ya Shilingi Bilioni 218, ambapo kati ya fedha hizo Shilingi Bilioni 62 sawa na 28.44% ya Bajeti yote ni kutoka kwenye vyanzo vya mapato ya ndani ya Halmashauri na Shilingi Bilioni 156 sawa na 71.56% ya Bajeti ni fedha za Ruzuku kutoka Serikali Kuu ambazo ni kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo na Matumizi ya kawaida.
Aidha, kikao hicho kilichofanyika kwenye ukumbi wa Mikutano wa Arnatouglou na kuongozwa na Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam Mhe. Omary Kumbilamoto, kilipitisha Mpango na Bajeti ya mwaka wa fedha 2021/2022 ambapo Bajeti ya Mapato ya ndani ya Halmashauri ya mwaka wa fedha 2021/2022 imeongezeka kwa 3.3% ukilinganisha na Bajeti ya Shilingi Bilioni 60 ya mwaka 2020/2021, hii imetokana na mikakati bora iliyowekwa na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa kukusanya mapato ya uchangiaji Huduma za Afya katika Hospitali mpya ya Kivule na Zahanati 3 mpya za Luhanga, Lubakaya na IDC Kliniki.
Katika kuandaa Mpango na Bajeti ya mwaka wa fedha 2021/2022 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imezingatia Mwongozo wa uandaaji wa Bajeti uliotolewa na Hazina Mwezi Februari, 2021, Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya Mwaka 2020, Hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli aliyoitoa wakati wa kuzindua Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jijini Dodoma la tarehe 13 Novemba, 2020.
Sambamba na hayo, lakini pia uandaaji wa mpango na bajeti umezingatia Sheria ya Bajeti Na. 11 ya mwaka 2015 sura 439 pamoja na kanuni zake, Mkakati wa Taifa wa Mapambano dhidi ya rushwa, Malengo ya Mellania (SDGs 2030) Mpango Mkakati wa Halmashauri 2017/2018 mpaka 2021/2021, Maoni ya wadau mbalimbali wa Halmashauri ambao wameshiriki katika maandalizi ya bajeti hii kuanzia ngazi ya Mtaa, Kata, Idara hadi Halmashauri kwa ujumla kwa kutumia mfumo wa Frursa na Vikwazo (O & OD iliyoboreshwa)
Aidha, katika makisio ya mpango na bajeti ya mwaka 2021/2022 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imejiwekea vipaumbele kumi na moja (11) pamoja na mikakati saba (7) itakayosaidia kufanikisha ukusanyaji wa mapato ya ndani ya Halmashauri ili iweze kutekeleza Mpango na Bajeti ya mwaka wa fedha 2021/2022
Makisio ya Mapato ya Ndani ya Halmashauri kwa mwaka 2021/2022
Kwa mwaka wa fedha 2021/2022 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imepanga kukusanya Shilingi Bilioni 62 kutoka kwenye vyanzo vyake 24 vya ndani
Matumizi ya Mapato ya Ndani ya Halmashauri kwa mwaka 2021/2022
Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa mwaka wa fedha 2021/2022 kwenye Mapato yake ya Ndani inatarajia kutumia fedha kiasi cha Shilingi Bilioni 62 katika mchanganuo ufuatao; Matumizi Mengineyo Shilingi Bilioni 18.184 sawa na 29.33% ya Bajeti, Mishahara Shilingi Bilioni 1.26 sawa na 2.03% ya Bajeti, Miradi ya Maendeleo Shilingi Bilioni 29.167 sawa na 47.04% ya Bajeti na Vyanzo Fungiwa Shilingi Bilioni 13.387 sawa na 21.59% ya Bajeti.
Makisio ya Fedha za Ruzuku kutoka Serikali Kuu
Ruzuku ya Shilingi Bilioni 156 kutoka Serikali Kuu imegawanywa katika maeneo mawili ambayo ni Matumizi ya Kawaida na Miradi ya Maendeleo
Mchanganuo wa Matumizi ya Kawaida kwa fedha ya Ruzuku
Kwa mwaka wa fedha 2021/2022 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam inatarajia kutumia Shilingi Bilioni 113.733 ya fedha ya ruzuku sawa na 72.9% kulipa Mishahara na Shilingi Bilioni 2.628 sawa na 1.68% kwa ajili ya Matumizi Mengineyo
Mchanganuo wa fedha za Miradi ya Maendeleo kwa fedha ya Ruzuku
Katika kipindi kijacho cha 2021/2022 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imepanga kutumia Shilingi Bilioni 39.642 kutekeleza Miradi ya Maendeleo ambayo ni sawa na 25.41%
Akiongea wakati wa kufunga kikao hicho cha Baraza la Madiwani, Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Mhe. Kumbilamoto alisema "napenda kuchukua nafasi hii kumshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kuipandisha hadhi Manispaa ya Ilala na kuwa Jiji la Dar es Salaam, niwaeleze tu, kwa mwaka uliopita, Halmashauri yetu imeongoza katika ukusanyaji wa mapato ghafi, lakini pia tumeweza kutoa mikopo ya 10% kwa mafanikio makubwa kuliko Halmashauri yoyote"
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.