Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita leo tarehe 24 Februari, 2018 amewasilisha mpango na bajeti ya mwaka 2018/2019 wa jumla ya shilingi bilioni 75.2 ikiwa ni bajeti ya mishahara ya watumishi, matumizi ya kawaida na za utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo.
Mpango na bajeti hiyo umepitishwa kwa kauli moja na wajumbe wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam huku wakimpongeza kwa kusema kuwa Jiji limepata Meya anayejali utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa ajili ya wakazi wa Jiji la Dar es Salaam.
Bajeti ya Halmashauri ya Jiji katika mwaka 2018/2019 imeandaliwa kwa kuzingatia Dira ya Maendeleo 2025, malengo endelevu ya millenia, Mpango wa maendeleo wa miaka mitano, Ilani ya Uchaguzi 2015-2020, Mwongozo wa bajeti wa mwaka 2018/2019, Hotuba ya Rais wakati wa ufunguzi wa Bunge na maelekezo mengine ya Serikali na Halmashauri ya Jiji.
Akizungumzia mpango na bajeti hiyo kwa wakazi na wadau mbalimbali wa Jiji waliohudhuria Mkutano wa Baraza, Meya Mwita amesema kuwa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imekadiria kukusanya na kutumia kiasi cha shilingi bilioni 75.2 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo kutoka mbalimbali vya mapato. Kati ya fedha hizo shilingi bilioni 18.1 zinatarajiwa kukusanywa kutoka kwenye vyanzo vya mapato ya ndani vya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam.
Aidha amefafanua kuwa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imeendelea kuboresha ukusanyaji mapato yake ya ndani pamoja na kubuni vyanzo vingine vya mapato.
Amefafanua kuwa mpango na bajeti ya mwaka 2018/2019 umelenga kutekelaza mradi wa ujenzi wa Kituo kipya cha Mabasi cha Mbezi Luis, kuboresha miundombinu ya Dampo, ujenzi wa vyoo vya Umma na kuhakikisha utoaji wa huduma unaoepusha usumbufu kwa jamii.
Amesema Halmashauri pia imepanga kutumia asilimia 65 ya mapato ya ndani sawa na shilingi bilioni 11.7 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo na shilingi bilioni 1.08 kwa ajili ya mfuko wa wanawake, vijana na walemavu.
Akizungumzia suala la utalii, Meya Mwita amesema kuwa katika bajeti hiyo zaidi ya shilingi bilioni 2 zimetengwa ili kuboresha sekta ya hiyo ikiwemo kununua mabasi, kutengeneza na kuboresha vivutio mbalimbali vilipo jijini hapa.
Ameongeza kuwa, kuboreshwa kwa sekta hiyo kutaongezea pato la Taifa pamoja na kutoa ajira kwa vijana waliosomea masuala ya utalii ambao kwa kiasi kikubwa hawana ajira.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.