Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam Mheshimiwa Omary Matulanga leo tarehe 27 Januari, 2021 amewaongoza wajumbe wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam katika ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Kituo Kikuu cha mabasi yaendayo mikoani na nchi za jirani kilichopo eneo la Mbezi Luis.
Akizungumza ndani ya eneo la mradi Meya Matulanga amesema ameridhishwa na maendeleo ya ujenzi kutokana na kukamilika kwa maeneo mbalimbali ya kutolea huduma ndani ya Kituo.
Meya Matulanga amepongeza juhudi za Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuwajali Watanzania katika kuboresha huduma mbalimbali za kijamii na kumshukuru kwa kutoa fedha za ujenzi wa Kituo hicho.
Mstahiki Meya Matulanga ametumia fursa ya ziara hiyo kwa niaba ya Madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam katika kuunga mkono kauli ya Waziri wa TAMISEMI Mheshimiwa Suleiman Jafo (Mb) juu ya mapendekezo ya kumuomba Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kituo hicho kuitwa jina la Rais John Pombe Magufuli.
Aidha ameeleza kutokana na kasi ya maendeleo ya ujenzi wa miundombinu mbalimbali iliyobakia, Kituo hicho kinatarajiwa kuanza rasmi kutoa huduma mwanzoni mwa Mwezi Februari, 2021.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.