Na.Rosetha Gange na Judith Damas
Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Amos Makala leo Mei, 31 2021 amefanya kikao kazi na Madiwani, wakuu wa idara, pamoja na watendaji kata katika ukumbi wa Arnatoglou uliopo Mnazi Mmoja Jijini Dar es Salaam lengo kubwa likiwa ni kufahamiana na kuwaelekeza vipaumbele vyake akiwa ni Mkuu mpya wa Mkoa wa Dar es Salaam ikiwemo usafi,utekelezaji wa ilani ya Chama, kutatua kero za wananchi,utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo,kuwapanga wamachinga pamoja na ulinzi na usalama.
Akizungumza katika kikao hicho Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Makala ameipongeza Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa kupata hati safi mara sita (6) mfululizo pamoja na kuwa vinara wazuri katika ukusanyaji wa mapato. Sambamba na hilo amewapongeza madiwani kwa kuwa wasimamizi wazuri katika kuhakikisha asilimia 10% ya pato la ndani ya Halmashauri inatengwa kwa ajili ya kuwawezesha wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kupata mikopo .
Aidha, Mhe. Makala amesisitiza suala la usafi katika Halmashauri ya jiji la Dar es Salaam kwani hali ya usafi katika Jiji hili hairidhishi hivyo amewataka watumishi pamoja na watendaji wa Kata kupanga mikakati ya haraka ili kulirejesha Jiji katika mandhari ya usafi kwani ndio kitovu cha wageni katika nchi yetu ya Tanzania.
“Jiji la Dar es salaam ni Jiji kubwa,watu mbalimbali wanafika hapa,Kwa hali ilivyo sasa hali si nzuri.Sijaridhishwa na hali ya usafi katika jiji la Dar es Salaam kwani hapa ndio uso wa Tanzania.Lazima jitihada za haraka zifanyike.”
Katika kuhakikisha suala hili linatekelezeka Mh.Makala amekusudia kuzindua kampeni ya usafi katika jiji la Dar es salaam na kuwasisitizia watendaji wote wa jiji wakawe wasimamizi wa zoezi hili na kuwa usafi uanze kwenye kaya,mitaa, kata na katika Halmashauri ya jiji lao.
Sambamba na hilo Mhe. Makala amesema kuwa atakuja na mpango wa kuwapanga upya wamachinga na wafanyabiashara ndogo ndogo katika jiji la Dar es salaam ili jiji liwe kwenye muonekano mzuri na liwe katika hali ya usafi. Pia amesisitiza kuwa kutokuwa na usimamizi na ufuatiliaji madhubuti kunafanya jiji kuonekana katika hali ya uchafu na wahalifu hutumia vibanda hivyo kama maficho yao wakati wa usiku.
Akitoa shukrani kwa niaba ya watendaji wote wa Jiji la Dar es Salaam Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam Mh.Omary Kumbilamoto alimpongeza Mh.Makala kwa hotuba nzuri na kuahidi kuyatekeleza yale yote aliyowaagiza na kumuhakikishia ushirikiano wa kutosha katika kutekeleza majukumu yake.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.