Mafunzo ya mfumo mpya wa Mipango na Bajeti (Planrep) yamezinduliwa leo Mkoani Mtwara kwa Waganga Wakuu, Makatibu wa Afya, Maafisa TEHAMA, Maafisa Mipango, Wahasibu, na Wachumi kutoka katika Mikoa ya Lindi, Mtwara, Ruvuma na Dar es Salaam.
Akifungua mafunzo hayo Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Mtwara Bw. Elias Nyabusami amesema mafunzo hayo yamekuja wakati muafaka na yatasaidia kuondoa changamoto mbalimbali zilizokuwa zikijitokeza katika mfumo wa zamani zikiwemo uwepo wa matoleo tofauti tofauti ya mfumo wa mipango na bajeti gharama kubwa zilizotumika pamoja na muda mrefu uliokuwa unatumika wakati wa kuandaa bajeti.
Akifafanua amesema kuwa mfumo huo mpya toleo la mtandao “Web based” utasaidia kutoa mrejesho wa mara kwa mara kwa ngazi husika za utawala kwa wakati na hakutakuwa tena na haja ya wahusika kusafiri kutoka katika vituo vyao vya kazi ili kushughulikia masuala ya Bajeti na Mipango kwa kuwa sasa yatafanyika katika Mikoa na Halmashauri husika na taarifa hizo kupatikana katika ngazi mbalimbali kwa njia ya mtandao wa intaneti.
Kwa upande wake Mkuu wa timu ya Rasilimali Fedha Kutoka mradi wa Uimarishaji wa Mifumo ya Sekta za Umma ujulikanao kwa Kiingereza kama “Public Sector Systems Streghthen (PS3)” Bw. Germini Mtei amesema kuwa kupitia mfumo mpya wa PlanRep Mipango yote na Bajeti za Vituo vya kutolea Huduma kwa wananchi itaonekana kupitia mfumo huo hali itakayosaidia kuongeza ufanisi, uwazi, uwajibikaji na kuboreshwa kwa utoaji huduma.
“Kwa kutumia mfumo huu mpya sasa tunaamini kuwa utasaidia kuondoa ucheleweshaji wa fedha kwenda kwenye miradi na upotevu wa fedha kwa kuwa kila kitu kitafanyika kwa njia ya mtandao” Alisisitiza Bw.Mtei.
Aliongeza kuwa mradi wa Uimarishaji wa Mifumo ya sekta za Umma (PS3) unafadhiliwa na Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani “USAID” ni wa miaka mitano, na utafanya kazi na Serikali Kuu pamoja na Halmashauri 93 katika mikoa 13 ya Tanzania bara katika maeneo yafuatayo:-
Aidha Afisa TEHAMA Mwandamizi toka Ofisi ya Rais TAMISEMI Bw. Archibold Kundasai amesema kuwa mipango yote kuanzia ngazi ya Kata, Halmashauri na Mikoa itakuwa katika mfumo huo na dhamira ya Serikali ni kuongeza tija katika kuwahudumia Wananchi kwa kuhakikisha kwamba mifumo yote ya TEHAMA inazungumza ili kubadilishana taarifa.
“Bajeti ilikuwa ikichukua muda mrefu kuandaliwa ambapo takribani miezi 4 ilitumika ambapo kwa mfumo huu tija itaongezeka kwa kuwa wahusika watabaki katika vituo vyao wakihudumia wananchi huku wakitekeleza jukumu la kuandaa Bajeti na Mipango yao” Alisisitiza Kundasai.
Serikali ya Tanzania na USAID kupitia mradi wa uimarishaji wa Mifumo ya Sekta za Umma (PS3) imeandaa mafunzo haya kwa watumiaji wake nchi nzima. Mafunzo yanatolewa na Wakufunzi kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI, Wakala ya Serikali mtandao, Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, Wizara ya Fedha na Mipango, Wizara ya Afya na unatarajiwa kutumiwa na watumiaji 1,500 watakaofundishwa matumizi ya mfumo huo.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.