MSTAHIKI Meya wa Jiji la Dar es Salaam Isaya Mwita leo tarehe 13 Julai, 2017 akiongozana na Waheshimiwa Madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam wamefanya ziara ya kutembelea miradi ya maendeleo ya jiji ambapo ameridhishwa na vikundi vinavyo tengeneza mkaa kwa kutumia taka kama malighafi na kueleza kwamba itasaidia kupunguza uchafu uliopo kwenye maeneo mbalimbali na kuliweka jiji katika hali ya usafi.
Ziara hiyo ambayo imehusisha Kamati ya Fedha ya Halmashauri ya Jiji, ilitembelea vikundi vya maendeleo ya ujasiriamali cha Upendo Smart kilichopo mtaa wa Kilimahewa Kata ya Tandika kinachojihusisha na uzalishaji wa mkaa mbadala (mkaa poa).
Aidha mbali na kikundi hicho Waheshimiwa Madiwani pia wamejionea shughuli za uzalishaji wa mkaa unaofanywa na kikundi cha maendeleo cha Mwangaza Vikoba kilichopo Pugu Stesheni jijini hapa.
Akizungumza na wanakikundi hao, Meya Mwita amesema kuwa vikundi hivyo vinafanya kazi kubwa kutokana na ubunifu walionao jambo ambalo litasaidia kuweka jiji kwenye hali ya usafi.
Alifafanua kuwa mbali na kuweka jiji safi pia litapunguza gharama kwa wananchi wanaotumia nishati ya mkaa kutokana na nishati hiyo kuuzwa kwa bei nafuu ukilinganishwa na ule unaotumika hivi sasa kwakuwa una gharama kubwa.
“Mmefanya kazi nzuri sana wakina mama nimeona juhudi zenu, lakini nimesikia changamoto kubwa hapa ni namna ya kuwafikia hao watu waweze kununua nishati hii, niwahakikishie Madiwani wenu wapo hapa, Meya wenu nipo hapa tutaendelea kuwaunga mkono” amesema Meya Mwita.
Aliendelea kueleza kwamba wananchi wanatumia gharama kubwa kununua mkaa unaochomwa kwa kutumia miti, lakini unapotumia huu ambao unatengenezwa na vikundi hivi, kwakutumia malighafi taka, unawezesha kuinua kiuchumi lakini pia tunatoka kwenye matumizi ya mazoea na kuingia kwenye matumizi ya kisasa.
Awali ziara hiyo ilianzia kwenye mradi wa ujenzi wa miundombinu ya viwanda vidogo vidogo katika eneo la karakana ya Mwananyamala ambapo lengo la mradi ni kuwafikishia huduma muhimu wanawake na vijana kwa pamoja ili wajikwamue kiuchumi, kujiongeza kipato na kupunguza tatizo la ajira hasa kwa vijana na kina mama kwa kuwarasimisha wajasiriamali hawa wadogo ambao wengi hawako rasmi kwa kukosa sehemu za kufanyia kazi.
Mradi huo unatokana na fedha zilizotengwa na Halmashauri ya Jiji katika bajeti ya mwaka 2016 /2017 katika kutekeleza azma ya Serikali ya Awamu ya Tano, inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ya kukuza uchumi wa nchi yetu katika maendeleo ya sekta za viwanda, biashara, masoko, viwanda vidogo, biashara ndogo na uwekezaji kwa kujenga miundombinu, majengo na maeneo ya huduma kwa ajili ya wajasiriamali wadogo kwa kushirikiana na Shirika la Viwanda Vidogo Vidogo (SIDO).
Awamu ya kwanza mradi huo utahusisha ujenzi wa majengo makubwa mawili yenye vyumba vitatu kila kimoja kwa ajili ya biashara umepangwa kutumia kiasi cha shilingi milioni 190, hadi kufikia mwisho wa mwezi Julai, 2017 utakuwa umekamilika kwa asilimia 82.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.