JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA

JIJI LA DAR ES SALAAM

Jiji la Dar es Salaam ni miongoni mwa majiji yanayokua kwa kasi barani Afrika huku kukiwa na ongezeko la watu. Miongoni mwa watu wanaoingia kwa wingi katika jiji hili ni vijana ambao kwa namna moja au nyingine wamekuwa na matumaini ya kufanikiwa kimaisha. Wengi wao wanapofika jijini hapa kutoka vijijini wanajikuta hawana shughuli rasmi ya kufanya, tofauti na matarajio yao kuwa kila kitu kitakuwa rahisi mara baada ya kutua katika jiji hili. Kutokana na kukosa matarajio yao wengi hujikuta wakiingia katika shughuli zisizo rasmi kama wachuuzi wa bidhaa za mikononi huku mtaji wao ukiwa ni uaminifu kutoka kwa watu wenye mali zinazotakiwa kuingizwa sokoni. Hata wanapofanikiwa kuaminiwa bado wanakuwa na tatizo la kupata sehemu maalumu ya kufanyia uchuuzi wao. 


HATUA ZILIZOCHUKULIWA NA HALMASHAURI YA JIJI

Jengo la Wafanyabiashara Ndogondogo (Business Park):

Mradi huu umebuniwa na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa lengo la kuwaweka pahala pamoja pa kufanyia kazi wafanya biashara ndogo ndogo zaidi ya 10,000 walio zagaa katika mitaa mingi ya katikati ya jiji letu. Lengo ni kuliweka jiji katika hali ya usafi na serikali kupata mapato yatokanayo na shughuli zinazofanywa na wafanya biashara hao.  

Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam katika kutekeleza dhamira yake kwa kushirikiana na ushirika wa wadau ili kuweza kutoa huduma bora za uhakika kwa wakazi wote wa Jiji la Dar es Salaam ili kupunguza umasikini na kukuza uchumi ilifikia makubaliano na shirika la taifa la hifadhi ya jamii (NSSF) mnamo mwaka 2007 ambapo NSSF walitoa fedha na kusimamia ujenzi wa jengo la mradi wa biashara wa Jiji (Machinga Complex)

Jengo la mradi wa biashara wa Jiji (Machinga Complex) linapatikana Mtaa wa Lindi, katika Manispaa ya Ilala lina uwezo wa kuchukua wafanyabiashara 4206.

Lengo kubwa la mradi huu ni kuwawezesha wafanyabiashara wadogo kufanya shughuli zao kwenye eneo rasmi na kuweza kukuza uchumi binafsi hatimaye waweze kukuza uchumi wa Taifa.

Vijana takribani mia tatu (300) kutoka vyuo mbalimbali vya taasisi za ufundi wamejiajiri ndani ya jengo la biashara la Machinga Complex.

Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam inawasisitiza wafanyabiashara wadogo kufanya shughuli zao rasmi kwenye jengo hili na kuondoka katika mitaa ya Dar es Salaam kwani jengo hili limejengwa kwa ajili yao.