JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA

JIJI LA DAR ES SALAAM

Usimamizi wa shughuli za dampo la kuhifadhi taka ngumu katika Jiji

Usimamizi na uendelezaji wa shughuli za dampo la kutupia taka ngumu katika Jiji la Dar es Salaam unafanywa na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam katika dampo lililopo katika eneo la Pugu Kinyamwezi katika Manispaa ya Ilala. Dampo hilo lina ukubwa wa hekta 65 ambao ni sawa na ekari 162.

Eneo hilo lilifanyiwa upembuzi yakinifu wa athari za mazingira, ”Environmental Impact Assessment,” na kuanza kutumika rasmi mwaka 2007 Halmashauri ya Jiji ilipokamilisha kuweka mipaka na kuweka miundombinu muhimu ya kufanikisha kazi ya kusafirisha taka kutoka maeneo mablimbali ya Jiji na kuzihifadhi katika eneo hilo.

Lengo la Halmashauri ya Jiji ni kujenga dampo la kisasa linalopaswa kukidhi matakwa yote ya kiafya na kimazingira, ”Sanitary Landfill”, ambalo lilikadiriwa kutumia kiasi cha shilingi bilioni tano. Uendeshaji wa madampo kwa teknolojia hii hutumika sehemu nyingi duniani hususan katika nchi zinazoendelea.

Kutokana na takwimu za Halmashauri ya Jiji za upokeaji wa taka katika dampo la Pugu Kinyamwezi, Jiji la Dar es Salaam linakadiriwa kuzalisha taka ngumu tani 4,252 kwa siku na kati ya hizo wastani wa tani 1,200 hadi 1,800 zinazolewa na kutupwa kila siku katika dampo hilo ambazo ni sawa na asilimia 43 hadi asilimia 48.

Wakati Halmashauri ya Jiji ikiwa inaendelea na juhudi za kupata fedha za kujenga dampo la kisasa linalopaswa kukidhi matakwa yote ya kiafya na kimazingira, kwa sasa inaendelea na uimarishaji wa huduma katika eneo hilo kwa upokeaji wa taka zinazosafirishwa kila siku katika dampo hilo, kuzipima kwa lengo la kuwa na takwimu za taka zinazoingizwa kila siku, kuzisambaza na kuzishindilia kwa udongo ili kupunguza harufu, mazalio ya inzi na  kuzuia uvujaji wa gesi unaosababisha kulipuka kwa moto.

Mara nyingi katika kipindi cha kiangazi kila mwaka, huwa kunatokea milipuko ya moto itokanayo na gesi ya taka “methane” inayojikusanya ndani ya dampo na kusababisha moshi mkubwa kusambaa kwenye eneo kubwa na kuleta kero kwa wakazi wanaoishi karibu na dampo la Pugu Kinyamwezi. Eneo hilo pia hunyunyiziwa dawa za kuua wadudu kama inzi, mbu, mende na panya mara kwa mara. Huduma hii huwasaidia pia wakazi wanaoishi jirani na dampo la Pugu Kinyamwezi.

Uchafuzi wa mazingira kwa maji machafu yanayotirikika ambayo husababishwa na kujichucha kwa taka hizo (Leachate) ni sehemu ya changamoto zinazoikabili Halmashauri ya Jiji katika eneo hilo. Kukabiliana na changamoto hizo Halmashauri inajenga eneo maalumu la kutupa taka(Cell) na bwawa la kuhifadhi maji machafu yanayotokana na kujichuja kwa taka (Leachate pond).

Kutokana na mvua kubwa zinazonyesha kila mwaka  na kuharibu kabisa barabara za kuingilia dampo zikisababisha magari kutoingia dampo kwa urahisi, Halmashauri ya Jiji imefanya ukarabati wa barabara za ndani ya dampo la Pugu Kinyamwezi kwa kiwango cha lami kwa kilometa 2.5 pamoja na ukarabati wa barabara ya kuingia katika dampo lenyewe kutoka katika barabara kuu iendayo Chanika kwa kilometa 0.7.

Kwa upande mwingine Halmashauri tayari imekwishajenga ukuta wa kuzunguka dampo hilo wenye urefu wa mita  1,020 ikiwa inaendelea na ujenzi huo kuzunguka eneo lote la ekari 162 kwa lengo la kuimarisha mipaka ya dampo na kuboresha miundombinu katika eneo hilo.

Kuharibika mara kwa mara kwa mitambo ya kusukuma taka pia imekuwa ni sehemu ya changamoto zinazoikabili Halmashauri ya Jiji katika upokeaji wa taka, usambazaji na ushindiliaji. Hatua zilizochukuliwa kukabiliana na changamoto hizo ni ununuzi wa mitambo “excavator, bulldozer na compactor dozer” ambayo kupatikana kwake kumeimarisha ufanisi katika shughuli za usimamizi na uendeshaji wa dampo la Pugu Kinyamwezi.

Kwa kuwa Halmashauri ya Jiji inakabiliwa na ufinyu wa fedha katika bajeti yake, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatoa ruzuku kila mwaka kuiwezesha Halmashauri hiyo kutekeleza majukumu yake kiufanisi katika usimamizi na udhibiti wa taka ngumu katika dampo la Pugu Kinyamwezi.