JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA

JIJI LA DAR ES SALAAM

Jitihada kubwa zinafanywa na Mamlaka za Serikali za Mitaa duniani kuiwezesha miji yao kuwa na uhusiano na miji mingine ndani na nje ya nchi zao. Uhusiano huo unaojulikana zaidi kama Uhusiano wa Miji Dada unaisaidia miji hiyo kushirikiana katika utekelezaji wa masuala mbalimbali ya kisiasa, kiuchumi na kijamii.


Lengo lake ni kuziimarisha Mamlaka za Serikali za Mitaa na wananchi wake katika sekta ya utoaji huduma kwa wananchi kwa kubadilisha uzoefu katika masuala ya utawala bora, uwajibikaji, ushirikishwaji wa wananchi katika maamuzi mbalimbali yanayohusu maendeleo na ustawi jamii. Kwa uhusiano huo pia imekuwa ikipata fursa ya kujadili mafanikio na changamoto mbalimbali zinazoikabili miji yao.


Jiji la Dar es Salaam ni miongoni mwa miji yenye Uhusiano wa Miji Dada na miji mingine ya nje ya nchi. Mwaka 2010 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam na Mamlaka ya Jiji la Hamburg (The Free and Hanseatic City of Hamburg) la nchini Ujerumani zilitia saini Mkataba wa kuwa na Uhusiano wa Miji Dada baina ya majiji hayo mawili yanayozungungwa na bahari.


Miji mingine yenye Uhusiano wa Miji Dada na Dar es Salaam ni kutoka nchini China ambayo ni Yiwu, Changzhou, Shaoxing, Jinhua na Beijing. Dar es Salaam pia ina uhusiano huo na Jiji la Lansing la nchini Marekani na Tswane, Afrika Kusini.

    

Kupitia uhusiano huo, Dar es Salaam imeweza kushirikiana na miji hiyo kuimarisha huduma zake za afya, zimamoto na uokoaji, maji, elimu, mazingira na huduma za bandari. Baadhi ya taasisi za Serikali zinazotoa huduma mbalimbali, asasi za kiraia, mashirika ya kidini ni miongoni mwa wadau wanaohusika moja kwa moja katika Uhusiano wa Miji Dada.


Katika Jiji la Hamburg Mamlaka ya Jiji hilo kwa kuzingatia matakwa ya wananchi ilibadilisha jina la mojawapo ya maeneo yake na kuliita eneo hilo Dar es Salaam Platz ikiwa ni hatua mojawapo ya kuimarisha uhusiano wa majiji hayo. Kwa upande wake Dar es Salaam pia ilibadilisha jina la Garden Avenue na kuwa Hamburg Avenue kwa lengo hilo hilo la kuimarisha uhusiano wake na Hamburg.


Kutoka Changzhou na Shaoxing nchini China, Jiji la Dar es Salaam lilifanikiwa kupata misaada ya pikipiki za kuimarisha huduma za usafiri wa kuwafikia wananchi ili kuweza kutoa huduma mbalimbali katika kata na mitaa.