Monday 6th, January 2025
@Viwanja vya Mnazi Mmoja
Kila tarehe 5 Juni, kila mwaka Watanzania tunaungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha Siku ya Mazingira Duniani. Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yaliamuliwa na Baraza la Umoja wa Mataifa la mwaka 1972, wakati wa mkutano wa kwanza wa Umoja wa Mataifa uliohusu Mazingira huko Stockholm, nchini Sweden.
Aidha, Azimio la kuunda Shirika la Umoja wa Mataifa la kushughulikia Mazingira Duniani, yaani United Nations Environment Programme (UNEP) lilipitishwa pia siku hiyo. Tangu wakati huo, nchi mbalimbali duniani zimekuwa zikiadhimisha Siku ya Mazingira Duniani kila mwaka tarehe 5 Juni, kwa ujumbe maalumu unaotolewa na Umoja wa Mataifa.
Madhumuni ya maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani ni kuhamasisha jamii duniani kote kuelewa masuala yahusuyo Mazingira na pia kuhamasisha watu wa jamii mbalimbali duniani kuwa mstari wa mbele katika kuchukua hatua za kuhifadhi na kulinda mazingira. Aidha, tunatumia siku hii kutoa fursa kwa jamii kufahamu kwamba wao wana wajibu wa kuzuia madhara na mabadiliko hasi katika Mazingira na kuhamasisha jamii kufanya mazingira yao kuwa salama na masafi katika maisha yetu na vizazi vyetu.
Kimataifa maadhimisho haya yanafanyika katika mji wa Hangzhou nchini China na kaulimbiu ya Kimataifa inayoongoza maadhimisho haya ni “Uchafuzi wa Hewa” (Air Pollution). Kaulimbiu hii inahimiza jamii kuepuka shughuli zinazo sababisha uchafuzi wa hewa. Maamuzi ya kupeleka maadhimisho haya China ni kutokana na nchi ya China kuwa na viwanda vingi ambavyo uzalishaji wake unasabisha uchafuzi wa Hewa. Hivyo, maadhimisho haya yanatoa fursa kwa nchi ya China na nchi nyingine duniani kuhamasika kuepuka shughuli zinazosababisha uchafuzi wa mazingira na kuwaepusha watu wake na maradhi yatokanayo na uchafuzi wa hewa.
Mwaka huu hapa nchini hatutakuwa na maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Mazingira Duniani na badala yake kila Mkoa utafanya shughuli za maadhimisho katika maeneo yake kwa kuzingatia kaulimbiu ya maadhimisho haya isemayo: “Tumia mifuko mbadala wa Plastiki; kwa ustawi wa Afya, Mazingira na Maendeleo ya Uchumi”. Kaulimbiu hii ni mwitikio wa Taifa wa Tamko la Serikali la kukataza uzalishaji, uingizaji ndani ya nchi usambazaji na matumizi ya mifuko ya plastiki na kuhimiza wananchi kutumia mifuko mbadala. Tamko hili limetokana na uharibifu mkubwa wa mazingira unaotokana na utupaji ovyo wa mifuko ya plastiki ambayo imeleta madhara makubwa ya kimazingira, afya za viumbe hai, ikiwemo binadamu wanyama, pamoja na kuathiri uchumi wa nchi kwa ujumla. Aidha, mifuko ya plastiki imekuwa sehemu muhimu ya jamii yetu, lakini changamoto ya usimamizi na athari za taka za plastiki nchini na duniani inahatarisha mustakabali wa ustawi wa jamii, uchumi na mazingira kwa kuwa mifuko hii huchukua muda wa takriban miaka 500 kuoza.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.