Na: Shalua Mpanda
Katika kuelekea Uchaguzi mkuu wa mwaka huu, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imeanza maandalizi kwa mafunzo ya maafisa uandikishaji majimbo pamoja na maafisa toka Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi kuhusu uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura yaliyoanza leo hii Machi 10, 2025.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo,Afisa Mwandikishaji wa Jiji hili Wakili Faraja Nakua amesema mara baada ya Watendaji hao kula kiapo cha utii na kuanza mafunzo hayo leo na kesho,yatafuata mafunzo kwa waandishi wasaidizi na BVR Opareta Machi 14 na 15 mwaka huu.
Aidha, amesema mara baada ya zoezi hilo la mafunzo kwa waandikishaji wasaidizi,kutafuatiwa na zoezi la usambazaji wa vifaa (BVR) katika kata zote 36 za majimbo matatu ya Uchaguzi ya Wilaya ya Ilala.
Afisa huyo Mwandikishaji amesema mara baada ya zoezi la usambazaji wa vifaa hivyo kukamilika siku ya Jumapili Machi 16, zoezi zima la uboreshaji wa Daftari la Kudumu kwa wapiga Kura litaanza rasmi Machi 17 hadi 23 katika Halmashauri nzima ya Jiji la Dar es Salaam.
"Nitoe Rai kwa wakazi wa Jiji la Dar es salaam kujitokeza kwa wingi katika maeneo yao kuhakiki taarifa zao katika zoezi hili muhimu ambalo litadumu kwa muda wa siku saba tu kuanzia tarehe 17 ya mwezi huu wa tatu". Alisema Wakili Nakua
Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wamesema wamejiandaa vyema kuhakikisha zoezi hilo linafanikiwa kwa asilimia 100 ili kuwawezesha wananchi kupata fursa ya kushiriki Uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka huu.
Zoezi hili la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ni maandalizi ya kuelekea katika Uchaguzi mkuu wa Rais,Wabunge na Madiwani kwa mwaka huu ambao umebeba ujumbe usemao "Kujiandikisha kwa Mpiga kura ni Msingi wa Uchaguzi Bora".
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.