Katika kutekeleza agizo la Serikali la kuhakikisha wananchi wanapata elimu ya mfumo mpya wa uombaji na utoaji wa mikopo kwa njia za Kibenki, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kupitia Idara ya Maendeleo ya Jamii leo Oktoba 29, 2024 wamefanya semina ya utoaji wa elimu ya mikopo ya asilimia 10 ya Halmashauri kwa wananchi wa Kata ya Ilala yenye lengo la kuwaelekeza sheria na kanuni za uombaji mpya wa mikopo ya asilimia 10 kwa vikundi vya Wanawake, Vijana na Watu wenye ulemavu kwa njia za kibenki.
Akiongea na wananchi hao, Afisa Maendeleo wa Jiji la Dar es Salaam Bi. Magreth Mazwile ameeleza kuwa lengo la semina hiyo ni kuhakikisha wananchi wanapata elimu juu ya mfumo mpya wa uombaji wa mikopo lakini pia kufahamu kanuni na taratibu za mikopo hiyo ili kuweza kuunda vikundi na kuomba mikopo hiyo isiyo na riba na yenye lengo la kuwakwamua Kiuchumi.
Aidha, Bi. Mazwile alisisitiza umuhimu wa vikundi kufuata taratibu zote muhimu katika kuomba mikopo hiyo, ili kuhakikisha wanapata fursa hii muhimu kwa maendeleo yao kwani mikopo hii haina riba na inalenga kusaidia vikundi kuanzisha au kuimarisha miradi ya kijasiriamali, na hivyo kuchangia katika kuleta maendeleo endelevu katika jamii huku akitoa wito kwa wananchi kujitokeza kuomba mikopo hiyo na kwa wale ambao bado hawajarejesha warejeshe kwa wakati ili na wanufaika wengine waweze kupata.
Katika Semina hiyo mada mbalimbali ziliwasilishwa pamoja na wananchi hao kufundishwa namna ya kuunda vikundi na kuvisaji ili kuweza kupata mikopo isiyo na riba itakayowaongezea kipato kwakuwa mikopo ya awamu hii imelenga kumfikia kila mnufaika kuanzia wafanya biashara wadogo wadogo pamoja na Mama lishe/ Baba lishe.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.