Leo tarehe 25 Novemba, 2022 Ubalozi wa China Nchini umekabidhi vifaa na vitendea kazi kwa shule jumuishi ya Uhuru Mchanganyiko ikiwa ni muendelezo wa ushirikiano baina ya Tanzania na China.
Akiongea kwa Niaba ya Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Mwl. Hamisi Mlangala aliushukuru ubalozi wa China nchini na kuwaomba kuendelea kutoa misaada kwani wanafunzi bado wana uhitaji.
"Tunashukuru Ubalozi wa China kwa kuweza kuona umuhimu wa kuwasaidia wanafunzi hawa. Huu ni moyo thabiti kutoka kwao na haya ni matunda yanayotokana na ushirikiano kati ya Nchi za Tanzania na China ambao Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ameendelea kuudumisha."
Nae Balozi wa China nchini Bi. Chen Mingjian ameoneshwa kufurahishwa na ushirikiano baina ya pande hizo mbili na kusema kuwa Ushirikiano wa Tanzania na China ni wa muda mrefu na wanajivunia kuuendeleza.
"Historia ya China na Tanzania imeanza miaka mingi iliyopita na mpaka sasa ushirikiano huu unazidi kudumishwa na hii ndio maana pia sisi tupo hapa kuudumisha. Siku kadhaa zilizopita Rais wa Jamhuri Mhe. Samia Suluhu Hassan alienda Nchini China na safari yake ilizidi kudumisha ushirikiano huu na pia makubaliano mengi yalifikiwa katika safari hiyo" aliongeza Bi. Mingjian
Aidha, Afisa Elimu Msingi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam Bi. Sipora Tenga alihitimisha kwa kusema "Tunashukuru na tumefurahi sana kwa Ubalozi wa China kwa msaada wa vifaa ambavyo vitawasaidia wanafunzi hawa. Tunatoa wito zaidi kwa wadau wengine waweze kujitokeza kwani tunawahitaji wote wenye nia njema kuunga mkono juhudi za Serikali ya awamu ya Sita kuwahudumia watoto."
Vifaa ambavyo vimetolewa ni pamoja na dawa, mito, sare za shule na sabuni ikiwa sehemu ya kuwainua kielimu wanafunzi.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.