Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Albert Chalamila amewataka wafanyakazi wote wa Mkoa wa Dar es Salaam kuwa watendaji wema na wazalendo katika maeneo yao ya kazi ili matarajio ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kutoka kwao yaweze kutimia.
Mhe. Chalamila ameyasema hayo Leo Tarehe 1 Mei, 2024 alipokuwa akiwahutubia wafanyakazi kutoka taasisi na mashirika mbalimbali kwenye maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani ambayo kwa Mkoa wa Dar es Salaam yamefanyika katika uwanja wa Uhuru uliopo Halmashauri ya Manispaa ya Temeke.
Akijibu hoja mbalimbali zilizotolewa na vyama vya wafanyakazi kuhusiana na maslahi yao, Mhe. Chalamila amesema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amekwishatoa maelekezo kwa wakuu wote wa Taasisi za Umma na Mashirika kufanya maboresho makubwa ili watumishi walitumikie taifa lao bila kuwa na malalamiko.
"Kuhusiana na Kodi Mhe. Rais alifanya maboresho lakini bado yamekuja maombi ya kushusha tena kutoka 9% kwenda angalau 3% ,haya yote viongozi wetu wameyachukuwa na wanayafanyia kazi. Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Msikivu kwa watumishi wa Taifa lake, Jambo lolote linaloibua majonzi na machozi kwao lazima atalifanyia kazi kwa masilahi bora ya watumishi,ili waweze kufanya kazi zao vizuri." Amesema Mhe. Chalamila
Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani yamefanyika kitaifa katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid Jijini Arusha na kubeba kaulimbiu ya 'Nyongeza ya Mishahara Ni Msingi wa Mafao Bora na Kinga Dhidi ya Hali Ngumu ya Maisha' ambapo Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndiye aliyekuwa mgeni Rasmi.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.