Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira anayeshughulikia masuala ya Mazingira Bi.Christina Mndeme ametoa wito kwa mama lishe na Baba lishe kuokoa maisha yao kwa kutumia nishati safi ya kupikia ambayo itawaepusha na athari katika mfumo wa upumuaji pamoja na utunzaji wa mazingira.
Bi.Mndeme ameyasema hayo leo, Septemba 27, 2024 Jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya ugawaji wa majiko ya kupikia kwa mama na baba lishe wa Kisutu iliyoandaliwa na Kampuni ya Bakhresa yenye lengo la kuunga mkono jitihada za Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Akizungumza katika hafla hiyo Bi. Mndeme amesema, Rais Samia licha ya kuwa kinara wa Afrika kwenye kampeni ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, pia amedhamiria kuwaondoa kina mama na baba lishe wa Tanzania katika matumizi ya nishati isiyo safi na pia kuboresha hali zao kwa kutumia nishati safi ya kupikia ambapo hii inaendana na kampeni ya kumtua mama kuni kichwani.
‘‘Nipende kupongeza sana Makampuni ya Bakhera kwa kuibeba ajenda hii ya nishati safi ya kupikia kwani mmeonesha kwa vitendo kuhakikisha mnamuunga mkono Rais wetu katika kuhakikisha tunatunza mazingira kwa kutumia nishati safi ya kupikia ambayo itaepusha athari zote za kimazingira zitokanazo na matumizi ya nishati isiyo safi, hivyo nitoe wito kwa wadau wengine kuhakikisha wanashirikiana na sisi katika kutunza mazingira ili hadi kufikia mwaka 2034 asilimia 80% ya watu wawe wanatumia Nishati safi ya kupikia."
Sambamba na hilo, Bi. Mndeme ameeleza kuwa matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa ujumla itaondoa uharibifu wa mazingira ambapo jamii itaachana na ukataji wa miti ovyo pamoja na kumtua mama kuni kichwani kwa kuwauondolea wanawake kutumia muda mwingi katika kutafuta kuni badala yake kufanya shughuli za Kiuchumi.
Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Maliasili na Uhifadhi wa Mazingira Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam Bi. Theresia Denis ameishukuru Kampuni ya Bakhressa kwa kuunga mkono juhudi za Mhe. Rais za kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia huku akieleza kuwa Jiji la Dar es Salaam litaendelea kuwa mstari wa mbele kuhakikisha wananchi wake wanatimia nishati safi ya kupikia ili kuondokana na athari za kimazingira na kuendelea kulinda mazingira na afya kwa ujumla.
Naye Meneja wa Uhusiano na Mawasiliano wa Makampuni ya Bakhressa Bi. Rehema Salim ameeleza kuwa katika kurudiasha fadhila kwa jamii Kampuni ya Bakhresa imeona ni vyema kuunga mkono juhudi za Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassani za matumizi ya nishati safi ya kupikia ambapo wameanza kwa kugawa majiko 60 kwa mama lishe na baba lishe wa Kisutu huku akieleza kuwa kampeni hii ni endelevu na itafanyika nchi nzima.
Aidha, mkakati wa matumizi ya nishati safi ya kupikia, ulizinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan, Mei 8, 2024 ukilenga kuepuka athari za matumizi ya kuni na mkaa unaoambatana na utunzaji wa mazingira.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.