Watumishi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam leo tarehe 22 Juni, 2020 katika kuhitimisha maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma watembelea ujenzi wa miundombinu ya Kituo Kikuu cha Mabasi yaendayo mikoani na nchi jirani katika eneo la Mbezi Luis jijini Dar es Salaam.
Katika ziara hiyo watumishi wamepata fursa ya kujionea hali ya utekelezaji wa mradi huo ambao ujenzi wake ulianza Januari, 2019 na hadi sasa umefikia asilimia 70 ya utekelezaji wake.
Ujenzi wa mradi wa kimkakati wa stendi ya mabasi katika eneo la Mbezi Luis ni juhudi za Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mhe. Rais John Pombe Magufuli katika kuboresha sekta ya usafiri na usafirishaji jijini Dar es Salaam ambapo Serikali Kuu imeipatia Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam fedha kiasi cha Shilingi za Kitanzania bilioni 50.9 kwa ajili ya utekelezaji wa ujenzi wa miundombinu ya Kituo Kikuu cha Mabasi yaendayo mikoani na nchi jirani cha Mbezi Luis.
Watumishi hao pia wamepata fursa ya kutembelea Kituo cha kulea na kuwahifadhi wazee kilichopo Nunge katika Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni na kutoa msaada mbalimbali ikiwemo vyakula, sukari, sabuni, mafuta ya kupikia, mafuta ya kupaka ngozi, maji na mashuka.
Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma husheherekewa mwezi Juni kila mwaka na kauli mbiu ya mwaka 2020 ni: “JUKUMU LA UTUMISHI WA UMMA KATIKA KUJENGA NA KUDUMISHA AMANI ILIYOPO MIONGONI MWA JAMII”
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.