Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Albert Chalamila amewahimiza maafisa ustawi kuhakikisha wanatoa elimu kwa Jamii juu ya masuala ya ukatili wa kijinsia na kuhakikisha wanakemea vitendo hivyo, hayo ameyabainisha Leo Agosti 6,2024 wakati wa ufunguzi wa mkutano wa Maafisa Ustawi wa Jamii Mkoa unaofanyika katika Ukumbi wa Karimjee Jijini Dar es Salaam ambao unatarajiwa kuhitimishwa Agosti 7, 2024 lengo likiwa ni kutoa fursa kwa Maafisa Ustawi wa Jamii kubadilishana uzoefu, kujifunza na kuunda mtandao wa ushirikiano ambao utasaidia katika kuboresha huduma za kijamii nchini pamoja na kukemea vikali vitendo vya ukatili wa kijinsia na taharuki za utekaji zisizo za kweli zinazoendelea kwenye jamii.
Akizungumza wakati wa ufunguzi huo, Mhe. Chalamila ameeleza kuwa Sekta ya Ustawi wa Jamii ni sekta muhimu sana kwa Jamii kwani inamuhusu mwananchi moja kwa moja hivyo kutokana na umuhimu wa sekta hiyo kumesababisha kuanzishwa kwa vyombo vya habari kwakua dunia ya sasa mambo mengi yanayoendelea huonekana sana mtandaoni hivyo, vyombo hivi vya habari vitakuwa ni chanzo cha kufikisha taarifa na elimu kuhusu ustawi wa jamii kwa wakati husika.
Sambamba na hilo, Mhe. Chalamaila amezindua channel maalum ya mtandaoni ya ustawi wa jamii iitwayo "Ustawi wa Jamii Dsm Digital" iliyoambatana na kukabidhi vifaa vya kuchakata habari ikiwemo kompyuta mpakato (laptop), kamera na vifaa vingine vitakavyotumiwa na vitengo vya ustawi wa jamii katika Halmashauri za Manispaa zote za Mkoa wa Dar es Salaam.
Halikadhalika, Mhe. Chalamila amewataka Maafisa Ustawi wa Jamii kufanya kazi kwa bidii na weledi mkubwa ili kuhakikisha huduma bora zinawafikia wananchi wote huku akisisitiza kuwa Serikali itaendelea kutoa ushirikiano na rasilimali muhimu kwa maafisa hao ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Aidha, Mhe. Chalamila alikabidhiwa tuzo ya kutambua mchango wake katika ustawi wa jamii na kupata fursa ya kutoa tuzo kwa Katibu Tawala wa Mkoa Dkt. Toba Nguvila, Mganga Mkuu wa Mkoa Dkt. Mohammed Mang'una pamoja na viongozi wengine kwa kutambua mchango wao katika sekta hiyo.
Awali Akiongea kwa Niaba ya Wakurugenzi wote wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam Tabu Faith Shaibu amewahimiza Maafisa Ustawi wote wa Mkoa kuhakikisha wanatumia vizuri fursa hiyo ya vyombo vya habari kwani vyombo vya habari ni muhimili muhimu sana katika kuhabarisha Umma.
“Hatua hii ni muhimu sana kwa kutambua vyombo vya Habari kwani kupitia vyombo hivi naamini watu watapata elimu ya kutosha na sisi tutao ushirikiano wetu kuhakikisha jambo hili linafanikiwa katika Mkoa wa Dar es Salaam pia niwasihi Maafisa Ustawi wa Jamii kutumia fursa hii kwani vyombo vya habari ni muhimili mkubwa wa kutoa taarifa kwa umma hivyo tuvipe kipaumbele ili tuweze kufikia lengo hivyo tunatoa Shukrani zetu kwa Mkuu wa Mkoa kutuzindulia vyombo hivi hivyo tupo tayari kupokea maelekezo yako ili kuleta ufanisi katika Mkoa wetu wa Dar es Salaam”. Amesema Bi. Shaibu.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Postal Address: S.L.P 20950
Telephone: 0738 378 386
Mobile: 0738 378 386
Email: info@dcc.go.tz
Copyright © 2017 Dar es Salaam City Council . All rights reserved.