Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Utatibu Mhe. William Lukuvi (Mb) ameipongeza Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa usimamizi mzuri wa miradi ya Maendeleo inayotekelezwa ndani ya Halmashauri huku akiagiza majengo ya ghorofa yawekwe lifti kwaajili ya kuwasaidia watu wenye uhitaji.
Mhe. Lukuvi amebainisha hayo leo Oktoba 9, 2024 wakati akiweka jiwe la msingi Mradi wa ujenzi wa vyumba vya madarasa 20 ya ghorofa Shule ya Sekondari Liwiti unaotekelezwa kwa awamu ya pili.
Akiongea mara baada ya ukaguzi wa majengo hayo, Mhe. Lukuvi ameipongeza Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa usimamizi na utekelezaji mzuri wa miradi huku akiwasisitiza Wanafunzi kuwa na maadili mema.
"Nitoe pongezi zangu kwa Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mkurugenzi wa Jiji, Madiwani pamoja na Wataalamu wote kutoka Jiji la Dar es Salaam kwa usimamizi mzuri wa miradi kwani Serikali ya awamu ya sita imelenga kuleta mabadiliko kwenye kila sekta hivyo tuendelee kutekeleza ilani, pia pamoja na kuweka jiwe la msingi madarasa hayo naelekeza madarasa hayo yawekwe lifti kwaajili ya kusaidia watu wenye uhitaji."
Sambamba na hilo, Mhe. Lukuvi amewataka Walimu na Wanafunzi kuwa na Maadili mazuri katika kuhakikisha watoto wanakua katika maadili bora na ufaulu unaongezeka ili kutimiza adhma ya Mhe. Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha watoto wanapata elimu bora na sekta ya elimu nchini inakua kwa kasi zaidi.
Awali akitoa taarifa za ujenzi wa madarasa hayo, Afisa Elimu Sekondari Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam Mwl. Mussa Ally ameeleza kuwa mradi wa ujenzi wa madarasa kwa awamu ya pili ulianza kutekelezwa Februari 27, 2023 na ulitarajiwa kukamilika Februari 26, 2024 ila kutokakana na ongezeko la kazi, mradi huo unatarajiwa kukamilika Disemba, 2024 na utagharimu kiasi cha shilingi bilioni 1.7 pindi ukikamilika huku akimshukuru Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuleta fedha kwaajili ya uboreshaji wa miundombinu ya sekta ya Elimu na sekta nyingine.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Postal Address: S.L.P 20950
Telephone: 0738 378 386
Mobile: 0738 378 386
Email: info@dcc.go.tz
Copyright © 2017 Dar es Salaam City Council . All rights reserved.