Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Albert Chalamila amewataka wakazi wa Mkoa huo na watanzania kwa ujumla kuyaishi na kuyatenda maono yote ya waasisi na mashujaa wa nchi yetu waliopigana na kuhakikisha wanaulinda Uhuru wa Nchi ya Tanzania.
Mhe. Chalamila ameyasema hayo leo Julai 25, 2024 kwenye maadhimisho ya kumbukumbu ya Mashujaa yaliyofanyika katika Viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama, viongozi wa kidini, viongozi wa Chama na Serikali pamoja na baadhi ya wananchi wa Mkoa wa Dar es salaam.
“Tunapozungumzia ushujaa kwa Taifa la Leo, tunapaswa kuyatenda na kuyaishi yale maono yote waliyokua nayo waasisi, wazalendo na mashujaa wa Taifa hili”. Amesema Mhe. Chalamila.
Aidha, ametoa Rai kwa watanzania wote kuendelea kuwa wazalendo kwa nchi yao na kuepukana na vitendo vya rushwa pamoja na Mambo yote yanayoweza kuhatarisha amani ya taifa letu.
RC Chalamila amesema, “Urithi mzuri waliotuachia mashujaa na wapigania uhuru wetu ni kuhakikisha taifa letu kinaendelea kuwa na Amani kwani ndiyo tunu muhimu inayoweza kutusaidia kuishi Kama ndugu na kuweza kuendeleza Taifa letu kwa namba linavyoendelea Sasa.”
Kumbukumbu ya siku ya mashujaa huadhimishwa kila ifikapo tarehe 25 Julai ya kila mwaka kwa kuwakumbuka mashujaa walioupigania, kuutetea na kuulinda uhuru wa nchi yetu ambapo mwaka huu kwa Mkoa wa Dar es Salaam yamefanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja na Kitaifa yamefanyika Dodoma ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alikuwa mgeni Rasmi.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Postal Address: S.L.P 20950
Telephone: 0738 378 386
Mobile: 0738 378 386
Email: info@dcc.go.tz
Copyright © 2017 Dar es Salaam City Council . All rights reserved.