Wakazi wa Jiji la Dar es Salaam wahimizwa kutumia nishati mbadala ya kupikia lengo likiwa ni kuunga Mkono Juhudi za Mhe. Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ya utunzaji wa mazingira, Wito huo umetolewa na Afisa Tawala wa Wilaya ya Ilala Bi. Flora Mgonja kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Ilala wakati aliposhiriki katika maadhimisho ya siku ya Mazingira Duniani kwa Wilaya ya Ilala yaliyofanyika leo Juni 4, 2024 katika Viwanja vya MnaziMmoja Jijini humo yenye lengo la kuhamasisha jamii juu ya matumizi ya Nishati mbadala ikiwa ni muendelezo wa matukio yanayofanywa na Jiji la Dar es Salaam katika kuelekea siku ya Mazingira Duniani ambayo huadhimishwa Juni 5 ya kila Mwaka ikiambatana na kauli mbiu isemayo ‘Urejeshwaji wa Ardhi, ustahimilivu wa hali ya Jangwa na ukame’.
Akizungumza na Wadau pamoja na wananchi wote walioshiriki katika maadhimisho hayo Bi. Mgonja Amesema “Ninyi nyote mnafahamu ajenda ya Mhe. Rais ya kuhamasisha umuhimu wa nishati mbadala ili kuendana na changamoto ya mabadiliko ya tabia ya nchipamoja na changamoto za mazingira kwa ujumla. Hii ni ajenda ambayo Mhe. Rais ameibeba kwa dhati kabisa kuhakikisha tunaanza mchakato wa kuelimisha Watanzania ili kuondokana na nishati ambazo sio rafiki kwa mazingira, na kutumia zilizo rafiki kwa mazingira ili kutunza mazingira yetu na afya kwa ujumla.”
Sambamba na hilo, Bi. Mgonja ameendelea kusema Kaulimbiu ya Madhimisho ya siku ya Mazingira duniani inaakisi suala zima la utunzaji wa mazingira kwa kutumia nishati mbadala huku akiwataka wananchi hao kutekeleza kauli mbiu hiyo kwa vitendo wakianzia katika ngazi za familia bila kusahau kutumia nishati mbadala ili kulinda afya na ustawi wa mazingira kwa ujumla.
Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Udhibiti Taka Ngumu na Usafishaji Bw. Rajabu Ngoda ameeleza kuwa ameeleza kuwa matukio haya yanayofanywa na Jiji la Dar es Salaam kuelekea maadhimisho ya siku ya mazingira Duniani yamekua chachu ya kuleta mafanikio zaidi kwa Jiji la Dar es Salaam kuwa Safi kwani wananchi wameonekana kujitokeza kwa wingi katika matukio yaliyoanza kufanyika tarehe 30 ikiwemo zoezi la usafi, bonanza la michezo pamoja na midahalo juu ya utunzaji wa mazingira huku akiwataka wadau kushirikiana na Jiji la Dar es Salaam kutunza mazingira na kushikamana kufanya usafi kwa afya za wananchi wake.
Aidha, katika Hafla hiyo vyeti vya shukrani vilikabidhiwa kwa wadau mbalimbali ikiwa ni kutambua Mchango wao katika utunzaji wa mazingira kwa Jiji la Dar es Salaam.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Postal Address: S.L.P 20950
Telephone: 0738 378 386
Mobile: 0738 378 386
Email: info@dcc.go.tz
Copyright © 2017 Dar es Salaam City Council . All rights reserved.