Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam inatambua ongezeko la aina tofauti za taka ngumu zikiwemo za taka za majumbani, taka za viwandani na taka za Hospitali ambazo hutupwa maeneo mbalimbali na hivyo kuweza kusababisha uchafuzi wa mazingira (hewa, maji na Ardhi).
Jiji la Dar es Salaam linakadiriwa kuzalisha zaidi ya tani 4,600 za taka kwa siku. Kati ya hizo ni asilimia 45 hadi 50 tu zinazopokelewa katika dampo sawa na tani 1,200 – 2,000 ya taka zinazokisiwa kuzalishwa kwa siku ambapo taka zinazobaki huishia kwenye maeneo ya wazi, mitaro ya maji, barabara na makazi.
Hali ya usafi wa Jiji la Dar es Salaam hususani udhibiti taka ngumu ni tatizo la muda mrefu ambalo lina changamoto nyingi. Tabia iliyozoeleka miongoni mwa jamii ya utupaji ovyo wa taka katika maeneo yasiyostahili imechangia Jiji kuwa chafu. Kuzagaa kwa taka kunaweza kuwa kichocheo cha milipuko ya magonjwa kama vile kipindupindu na magonjwa mengine ya kuhara na kutapika. Hali ya uchafu Jijini inachangiwa pia na elimu ndogo juu ya usafi wa mazingira, kutotii sheria zilizopo kwa upande wa wananchi na usimamizi hafifu wa sheria za usafi wa mazingira.
Ili kupunguza uchafuzi wa mazingira, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imeandaa sera ya urejelezaji wa taka ngumu ambayo itakuwa ni msingi muhimu kwa Taasisi za Serikali kuanza kutambua na kurasimisha sekta ya urejelezaji taka ambayo awali ilikuwa ikiendeshwa na Taasisi binafsi na vikundi visivyokuwa rasmi.
Katika kuhakikisha hilo linafanyika Halmashauri ya Jiji la Dar Es Salaam inalenga kufanya yafuatayo;
Urejelezaji wa taka una faida nyingi miongoni mwa jamii kama; kuongeza thamani ya taka na kipato katika jamii, kupunguza malundo ya taka katika mitaa na maeneo ya jamii, kupunguza gharama za uendeshaji wa dampo, kupunguza gharama za udhibiti taka katika Manispaa na kuongeza uelewa wa jamii katika uchambuzi wa taka kuanzia ngazi ya kaya.
Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam inalenga kuhakikisha kiwango cha juu cha uzuiaji wa uchafuzi wa mazingira kwa kuweka taratibu zitakazowezesha aina nyingi za taka zinatakazozalishwa katika Jiji ziweze kurejelezwa (Recycling and Re-use) ili kuwa na Jiji safi.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Postal Address: S.L.P 20950
Telephone: 0738 378 386
Mobile: 0738 378 386
Email: info@dcc.go.tz
Copyright © 2017 Dar es Salaam City Council . All rights reserved.