Saturday 23rd, November 2024
@Mwananyamala
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mheshimiwa Paul Makonda, anatarajiwa kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa viwanda vidogo vidogo vinavyojengwa na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam katika eneo la Mwananyamala jijini Dar es Salaam ili kuwawezesha wajasiriamali kuboresha ustawi wa maisha yao. Tukio hilo litakalofanyika tarehe 09 Septemba, mwaka huu litahudhuriwa na Mameya wote wa Dar es Salaam, Waheshimiwa Madiwani wa Halmashauri ya Jiji, viongozi mbalimbali, wananchi na wajasiriamali zaidi ya 100.
Ujenzi wa viwanda hivyo ni sehemu ya utekelezaji wa Kauli Mbiu ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa John Pombe Magufuli, inayochochea uanzishwaji wa viwanda nchini kufikia malengo ya uchumi wa kati ambapo Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, pamoja na kuwawezesha wawekezaji wakubwa wa viwanda kufikia malengo yao na kuwajengea mazingira bora ya uwekezaji, imepanga kujenga viwanda vidogo vidogo kwa ajili ya akina mama, vijana na walemavu wa Jiji la Dar es Salaam pamoja na kuwapatia fedha za mikopo zinayotokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri.
Katika Mwaka wa Fedha 2016/2017, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ilitenga kiasi cha shilingi 200,000,000.00 kwa ajili ya ujenzi wa viwanda vidogo vidogo ambao utekelezaji wake ulianza tarehe 01 Juni, 2017 ambapo hadi kufikia mwezi Agosti, 2017 ujenzi wa miundombinu hiyo umefikia asilimia 95. Gharama za mradi huo ni shilingi 199,988,052.00. Ujenzi huo utaendelea kutekelezwa na Halmashauri ya Jiji katika Manispaa za Ilala, Kigamboni, Temeke na Ubungo kwa kadri maeneo yatakavyopatikana.
Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ambayo inashirikiana na Shirika la Kukuza Viwanda Vidogo Vidogo(SIDO) kuwajengea uwezo wajasiriamali hao itawawezesha kupata mafunzo yatakayowasaidia kuboresha zaidi uzalishaji na biashara zao. Kwa upande mwingine itakuwa rahisi zaidi kwao kupata mikopo kutoka kwenye taasisi za fedha, wadau mbalimbali pamoja na huduma muhimu kutoka Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Mamlaka ya Chakula na Dawa Nchini (TFDA) na wadau wengine.
Kwa kutumia vyombo mbalimbali vya habari vya ndani na nje ya nchi, tovuti ya Halmashauri pamoja na mitandao ya kijami, Halmashauri ya Jiji itawasaidia wajasiriamali hao kujitangaza zaidi ili waweze kupata masoko ya bidhaa zao ndani na nje ya nchi na inatoa wito kwa wajasiriamali wote watakaopata nafasi katika viwanda hivyo kuitunza miundombinu katika maeneo yote yatakayojengwa viwanda hivyo kwa maslahi ya wananchi wote.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.