Na: Shalua Mpanda
Afisa Mwandikishaji wa Jiji la Dar es Salaam Wakili Faraja Nakua amefungua mafunzo kwa waendeshaji wa vifaa vya Bayometriki na waandishi wasaidizi wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ngazi ya kata na kusisitiza mambo matano muhimu ili kufanikisha zoezi hilo.
Wakili Nakua amesema zoezi hilo la uboreshaji linalotarajiwa kuanza Machi 17, 2025 ni muhimu kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Rais,Wabunge na Madiwani unaotarajiwa kufanyika mwaka huu.
Amewataka Watendaji hao kuwa na weledi, nidhamui,kujituma kazini,bidii ya kazi pamoja na kuwa na lugha nzuri na zenye staha kwa "wateja" wao ambao ni wananchi.
"Wateja wetu Wapiga kura watakaojitokeza kujiandikisha kwa ajili ya kupiga kura,kuboresha taarifa zao au kuondoa taarifa za wapiga kura ambao hawana sifa za kuendelea kuwepo kwenye Daftari hilo,hivyo tunapaswa kuwa na lugha nzuri kwao na zenye staha".Alisisitiza Afisa huyo.
Aidha, amewataka waandishi na Waendesha Vifaa hao kufanya kazi kwa ushirikiano na wakala wa vyama vya Siasa katika vituo vyao na kutambua kuwa Wakala hao sio maadui bali ni wadau wanaowezesha zoezi hilo kukamilika.
Ameongeza kusema kuwa wanapaswa kuhakikisha wakala wa vyama hivyo vya Siasa hawavuki mipaka ya kazi yao.
Mafunzo haya ya Waendesha Vifaa vya Bayometriki na waandishi wasaidizi wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura yanafuatia mafunzo ya awali yaliyofanyika mapema wiki hii kwa Watendaji ngazi ya Jimbo na kuhudhuriwa na Mkurugenzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ndugu Ramadhan Kailima.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.