Na Doina Mwambagi
Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mhe. Edward Mpogolo, Leo tarehe 27 Januari amewataka wakazi wa wilaya hiyo kuendeleza uzalendo wa kweli kwa kutunza mazingira Kwa kupanda miti
Ameyasema hayo katika maadhimisho ya siku ya kuzaliwa ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, yaliyofanyika katika shule ya wasichana Jangwani Mhe. Mpogolo amesema kuwa uzalendo wa kweli huanzia katika vitendo vinavyolinda rasilimali za Taifa, hususan mazingira.
“Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa mstari wa mbele katika utunzaji wa mazingira. Hivyo, tunapoadhimisha siku ya kuzaliwa kwake, tunapaswa kufata maono yake kwa kupanda miti, kwani unapopanda mti unatunza mazingira na unaweka msingi wa maisha bora kwa kizazi kijacho,” amesisitiza Mkuu wa Wilaya.
Aidha, Mhe. Mpogolo ametoa wito kwa wananchi wa Ilala kuhakikisha kila kaya inapanda miti isiyopungua mitatu, huku akiwataka wakuu wa shule na Taasisi mbalimbali kusimamia ipasavyo upandaji na utunzaji wa miti ili kuhakikisha inaleta tija iliyokusudiwa.
Awali akimkaribisha mgeni rasmi, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Ndugu Elihuruma Mabelya, amesema kulingana na kaulimbiu “Uzalendo ni kutunza mazingira, shiriki kupanda miti”, Halmashauri imejipanga kupanda miti zaidi ya milioni moja katika maeneo mbalimbali ya jiji hilo, sambamba na kuimarisha utunzaji wa mazingira na matumizi ya nishati safi.
Maadhimisho hayo yamefanyika kufuatia agizo lililotolewa na ofisi ya Ikulu mnamo tarehe 22 Januari 2026, linaloelekeza kuwa siku ya kuzaliwa ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, idhimishwe kwa vitendo kwa kupanda miti kama ishara ya kuunga mkono utunzaji wa mazingira.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.