Jiji la Dar es Salaam na Jiji la Busan nchini Korea Kusini yanatarajiwa kuanzisha uhusiano wa miji dada ifikapo mwezi Mei, 2023. Azimio la kuanzishwa kwa uhusiano huo lilipitishwa tarehe 24 Februari, 2023 katika ukumbi wa mikutano wa Karimjee wakati mkutano wa pamoja kati ya wawakilishi wa Mamlaka ya Jiji la Busan, na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam.
Katika mkutano huo, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Mhandisi Amani Mafuru, alisema kuwa uamuzi wa kuanzisha uhusiano huo unatokana na juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dr. Samia Suluhu Hassan, kwa kufungua milango ya uhusiano kati ya Tanzania na nchi nyingi za nje.
"Tunamshukuru Rais wetu, Mheshimiwa Dr. Samia Suluhu Hassan, kwa kufungua milango na nchi za nje na kutumwezesha kuanzisha uhusiano na Jiji la Busan ambalo ni la pili kwa ukubwa nchini Korea Kusini," alisema Mhandisi Mafuru.
Kiongozi wa ujumbe wa watu wanne kutoka katika Mamlaka ya Jiji la Busan, Hwang Youngha, ambaye ni Mkurugenzi wa Diplomasia na Biashara alisema kuwa Jiji la Busan linapenda kutumia fursa ya kuanzishwa kwa uhusiano huo kushirikiana na Jiji la Dar es Salaam kuboresha na kuimarisha huduma katika sekta mbalimbali.
Sekta zilizojadiliwa na kukubalika na pande zote mbili ni elimu, afya, utalii, huduma za bandari, uvuvi na teknolojia ya habari na mawasiliano. Sekta zingine ni uboreshaji wa mazingira, udhibiti wa taka ngumu, ujenzi wa makazi ya kisasa, biashara na ziara za kujifunza namna ya kuimarisha ufanisi katika sekta mbalimbali.
Kabla ya mkutano huo uliokuwa na uwakilishi kutoka Ubalozi wa Korea Kusini nchini Tanzania, Mamlaka ya Bandari Tanzania, Wakala wa Meli na Vivuko Tanzania na wakuu wa Idara na vitengo wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, ujumbe huo wa kutoka Jiji la Busan ulipata fursa ya kukutana na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mheshimiwa Amos Makala anbaye aliridhia kuanzishwa kwa uhusiano wa miji dada kati ya Jiji la Dar es Salaam na Jiji la Busan.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.