Katika kuendeleza na kutekeleza kampeni ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe.Amos Makaka Mkuu wa Wilaya ya Ilala Leo Februari 25,2023 ameshiriki zoezi la usafi katika Kata ya Kariakoo ambapo usafi huo ulijumuisha maeneo ya Barabara ya Bibi Titi, Barabara ya Nkurumah pamoja na maeneo ya barabara ya Lumumba na Barabara ya Morogoro.
Zoezi hilo lililoongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Edward Mpogolo akiambatana na Katibu Tawala wa Wilaya ya Ilala, Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Diwani wa Kata ya Gerezani na Jangwani, Watumishi kutoka Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Watendaji wa Mtaa, viongozi wa Chama cha Mapinduzi wa Kariakoo Mashariki, viongozi kutoka shujaa wa maendeleo na Ustawi wa Jamii Tanzania (SMAUJATA), wadau kutoka Bank ya CRDB na wadau mbali mbali wa usafi wakiwemo Wejisa Company limited, Kajenjere Trading Company Limited, Sateki Trading Limited, Umoja wa Madereva wa Pikipiki Mjini Kati, Vingunguti na Msimbazi Jogging Club pamoja na Wananchi wa Kata ya Kariakoo.
Aidha, Mhe.Edward Mpogolo amewashukuru viongozi wa Machinga na Bodaboda kwa kuweza Kuhudumu katika Barabara ya Lumumba hivyo ameelekeza Vigingi na Miti kutoka barabara ya Airport vihamishwe na kuletwa barabara ya Lumumba ili kuboresha eneo hili.
“Kutokana na ukubwa wa Barabara ya Lumumba napenda kuwaomba watu wa maduka waboreshe maeneo yao huku upande wa katikati ya barabara tutahakikisha Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam tunashirikiana na Wamachinga, Bodaboda pamoja na wadau mbalimbali ili kuhakikisha barabara hii inakuaje safi na bora kwani Dar es Salaam hususani Wilaya ya Ilala kwani ndiyo Kitovu cha kupokea wageni wanaoingia Nchini.”
Sambamba na hilo Mhe. Mpogolo amemuelekeza Mkurugenzi wa Jiji kwa kushirikiana na watendaji wake kuhakikisha wanaandaa barua na Kuwapelekea wafanyabiashara wote wenye Majengo kuanzia barabara ya Airport hadi Ikulu ili kuona namna gani watawaelekeza kuboresha mazingira na miti gani waweze kupanda kwenye maeneo yao ili kuboresha mazingira ya Mji wetu.
Aidha Mhe. Mpogolo amewataka vijana wote wanaobandika stika maeneo ya Lumumba kuhakikisha wanaweka Jiji safi baada ya kumaliza kazi zao. Akiendelea kuongea katika zoezi Hilo Mhe.Mpogolo ameelekeza vifusi vyote vya mchanga vilivyopo barabarani kuondolewa pia watu wa ustawi wa jamii watafute namna ya kuwaelekeza watu wote wanaolala kando ya barabara na ndani ya Viwanja wahakikishe wanawaondoa katika maeneo hayo kwa kutumia utaratibu maalumu huku akiwataka wanaoegesha magari maeneo ambayo sio ya maegesho kupigwa faini kwani ni moja ya uchafuzi wa mazingira.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam Eng. Amani Mafuru ameeleza kuwa kampeni hii ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam imekua ya mafanikio zaidi kwa Jiji la Dar es Salaam kuwa Safi kwani wananchi wameonekana kujitokeza kwa wingi katika zoezi la usafi.
“Nipende kutoa Shukrani zangu za dhati kwa Mkuu wa Mkoa Wa Dar es Salaam Mhe.Amos Makalla kwa kuanzisha Kampeni hii ambayo ni endelevu kwani kutoka na kampeni hii Mkoa wa Dar es Salaam umeweza kushika nafasi ya Sita barani Afrika kwa usafi hivyo niwaombe wananchi kuhakikisha usafi ni Sehemu ya maisha yetu ya Kila siku na si mpaka tusubiri usafi wa mwisho wa mwezi.” Ameeleza Eng. Mafuru.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.