Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mhe. Edward Mpogolo, leo Julai 28, 2023, ameongoza kikao cha Tathmini ya Utekelezaji wa Mkataba wa Lishe kilichofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano DMDP chenye lengo la kupokea na kupitia utekelezaji wa Tathmini ya Hali ya Lishe kwa mwaka 2022/2023.
Akifungua kikao hicho, Mhe. Mpogolo amewataka wajumbe wa kikao hicho kufahamu kuwa lishe ndio msingi wa kila kitu na kwamba kikao hicho ni muhimu katika uboreshaji wa lishe katika jamii ili kuondokana na udumavu.
Sambamba na hilo, Mhe. Mpogolo amewaelekeza Wakuu wa Shule za Sekondari na Msingi kuendelea kuhakikisha wanatoa chakula mashuleni ikiwa ni sehemu ya kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambapo suala la lishe shuleni katika uongozi wa Awamu ya Sita ni kipaumbele.
"Mpaka sasa kwa ngazi ya Halmashauri tuna asilimia 98.02 ya Shule za Msingi na Sekondari zinazotoa chakula shuleni. Hivyo niwaase kuongeza juhudi ili tufikie asilimia 100. Pia walimu wasimamie uanzishwaji wa vilabu mashuleni kwani kwani itasaidia wanafunzi kupata uelewa zaidi juu ya masuala ya lishe." Amesema Mhe. Mpogolo
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam Ndg. Jomaary Satura amewataka Watendaji wa Kata kuhakikisha wanafanya ufuatiliaji wa afua za lishe, ili kujiepusha na kutia doa hatua nzuri ya hali ya lishe katika Jiji la DSM.
Awali, Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam Bi. Zaituni Hamza aliwasilisha taarifa ya utekelezaji ya tathmini ya Lishe kwa mwaka 2022/2023, ambapo katika taarifa hiyo amesema Kata zote 36 ndani ya Jiji la DSM zimefanikiwa kuadhimisha siku ya lishe ndani ya Kata.
Ikumbukwe kuwa moja ya vitu ambavyo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amevipa kipaumbele ni suala la Lishe bora nchini. Na hii ikiwa ni mkakati wa kuhakikisha nchi inaondokana na tatizo la utapiamlo na wananchi wake wanakuwa na afya bora na kuwawezesha kufanya kazi kwa bidi kwa maslahi mapana ya mwananchi mmoja mmoja na Taifa zima kwa ujumla.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.