Menejimenti ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam leo tarehe 6 Aprili, 2018 imefanya kampeni ya kukuza na kuendeleza utalii jijini kwa ufanya ziara ya kutembelea majengo na maeneo ya kihistoria, sehemu za kitamaduni, ngoma na sanaa za mikono kwa kutumia basi la utalii ambalo litakua linatembeza watalii wa ndani na nje ya nchi katika maeneo mbalimbali ya vivutio vya utalii jijini Dar es Salaam pamoja na Mji wa Bagamoyo.
Akiongea na waandishi wa Habari pamoja na wananchi mbalimbali katika katika ziara hiyo ya kutembelea vivutio vya utalii Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Bi. Sipora Liana amesema kazi ya kukuza na kuendeleza utalii jijini Dar es Salaam imeanza rasmi kwa kuhakikisha kwamba hamasa na elimu kwa jamii inatolewa ili kuwawezesha wananchi na wageni mbalimbali kutembelea maeneo ya utalii kwa ajili ya kujifunza lakini pia itakua ni hatua ya kujiongezea kipato kwa wafanya biashara mbalimbali.
Katika hatua nyingine Bi. Sipora amesema Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imepanga kuongeza usafiri wa kutembeza watalii jijini Dar es Salaam kwa kununua mabasi mengine ya utalii pamoja na bajaji za kitalii “luxurious bajaji” ambazo zitafanya shughuli za kutembeza watalii katika maeneo yote ya Jiji.
Ameongeza kusema kuwa wataenda mbali zaidi kwa kununua boti ambazo zitakua ni kivutio kikubwa kwa watalii kutembelea visiwa jirani vya Mbudya na Bongoyo na hata kufanya sherehe mbalimbali.
Aidha wakazi mbalimbali wa Jiji la Dar es Salaam wameipongeza Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa hatua hiyo ya kukuza na kuendeleza utalii jijini na kusema ni fursa nzuri kwao kwani itawawezesha kujifunza kuhusu historia ya Jiji la Dar es Salaam sambamba na kuwaongezea wigo wa kibishara na kuongeza pato binafsi na la TAIFA kwa ujumla.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.