Na: Doina Mwambagi
Katika kuadhimisha Wiki ya Upandaji Miti, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imeendelea kutekeleza juhudi za uhifadhi wa mazingira kwa kupanda miti katika maeneo mbalimbali, ikiwa ni sehemu ya mpango endelevu wa kuhakikisha mazingira yanabaki salama kwa kizazi cha sasa na kijacho.
Maadhimisho hayo ya wiki ya upandaji miti yamefanyika Leo tarehe 25 Machi 2025 katika shule ya msingi Uhuru mchanganyiko iliyopo Jijini humo.
Akiongea na wanafunzi, walimu na wadau wa mazingira mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya Kishe Adrian amesema anatambua jitihada zinazofanywa na Halmshauri ya Jiji la Dar es salaam katika kutunza mazingira kwa kuhamasisha wananchi matumizi ya nishati safi ya kupikia na kupanda miti
“Nawasihi tuendelee kutunza miti tuliyoipanda kwa sababu ni urithi wa kizazi kijacho. Tunapanda miti leo kwa ajili ya mustakabali wa baadaye.” Ndg. alisema Kishe.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo ambaye pia ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Bi Tabu Shaibu amesema Katika kuunga mkono juhudi za uhifadhi wa mazingira, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam inaendelea kusisitiza umuhimu wa upandaji na utunzaji wa miti kwa manufaa ya sasa na ya baadaye. Kupitia kaulimbiu “Ongeza thamani ya mazao ya misitu kwa uendelevu wa rasilimali kwa kizazi hiki na kijacho,” Jiji limejizatiti kuhakikisha miti inapandwa na kuhifadhiwa si tu kwa ajili ya kutoa hewa safi, bali pia kwa kuongeza thamani ya mazao yatokanayo na misitu kama mbao, matunda, na mimea dawa. Jitihada hizi zinahakikisha kuwa rasilimali za misitu zinatumika kwa uangalifu, huku kizazi cha sasa kikifaidi na pia kuwaachia urithi endelevu wale watakaokuja baadaye.
Awali akisoma risala kwa mgeni rasmi mkuu wa kitengo cha maliasili na uhifadhi wa mazingira Bi Teresia Denis amesema Halmashauri ya Jiji kwa miaka mitatu 2022-2025 imefanikiwa kupanda miti zaidi ya 2,149,601 katika maeneo mbalimbali ikiwemo shule, magereza, bonde la moto msimbazi na ufukweni.
Halmashauri ya Jiji imeahidi kuendelea kutekeleza mpango huu ili kufikia malengo yaliyowekwa na serikali, huku ikiwahimiza wananchi kushiriki kikamilifu katika juhudi hizi za kutunza mazingira kwa faida ya vizazi vijavyo.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.