Uchaguzi wa Naibu Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam umefanyika leo tarehe 07 Desemba, 2018 katika ukumbi wa Karimjee ambapo Wajumbe 24 wa Baraza la Madiwani wamekubaliana kwa kauli moja kuwa na Manaibu Meya wawili kutoka vyama vya CCM na Muungano wa Vyama vya Upinzani (UKAWA) ambao watahudumu katika awamu mbili za miezi mitatu kila mmoja.
Uamuzi huo uliafikiwa na Wajumbe wote wa Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kufuatia kuwa na idadi sawa ya wajumbe 12 kutoka Chama Tawala CCM na 12 kutoka UKAWA.
Akizungumza wakati wa kutangaza maamuzi yaliyoafikiwa kwa pamoja na Wajumbe wa Baraza hilo, Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam Isaya Mwita amesema kuwa kutokana na hali hiyo kila Naibu Meya ataaongoza kwa kipindi cha miezi mitatu kuanzia tarehe 30 Desemba, 2018 hadi ifikapo tarehe 30 Juni, 2019.
Manaibu Meya waliochaguliwa ni Mhe. Mariam Lulida, Diwani wa Kata ya Mchafukoge kwa tiketi ya CCM na Mhe. Ally Haroub Mohamed, Diwani wa Kata ya Makumbusho kwa tiketi ya CUF.
Uteuzi wa wajumbe wa Kamati za kudumu za Halmashauri ya Jiji, uchaguzi wa Wenyeviti wa Kamati hizo, kupokea taarifa za utekelezaji za Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam za mwaka wa fedha 2017/2018 pamoja na upitishaji wa ratiba ya vikao vya Halmashauri ni miongoni mwa ajenda zilizojadiliwa katika Mkutano Mkuu wa Halmashauri ambao wananchi na wadau mbalimbali wa Jiji la Dar es Salaam walihudhuria.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.