Katika kuendelea kutekeleza Mkataba wa Lishe katika jamii, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kupitia Idara ya Afya, Lishe na Ustawi wa Jamii leo Septemba 5, 2024 wamefanya mafunzo ya siku moja ya uhamasishaji wa Afua za lishe kwa Viongozi wa dini ikiwa ni mwendelezo wa utekelezaji wa agizo la Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan la kuhakikisha Jamii inafahamu umuhimu wa lishe ili kufikia adhma ya kuboresha Afya na ustawi wa Watanzania.
Akifungua mafunzo hayo kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Jiji la Dar es Salaam, Afisa Afya wa Jiji hilo Reginald Mlay amewahimiza viongozi wa dini kuendelea kutumia fursa ya majukwaa ya dini kuielimisha na kuihamasisha jamii juu ya masuala ya lishe kwa watoto wa chini ya miaka mitano pamoja na kuhakikisha wananchi wana mtindo bora wa maisha ili kufikia adhma ya kuboresha Afya na ustawi wa Watanzania.
“Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam inatambua nafasi na ushawishi mkubwa wa viongozi wa dini katika jamii na ndio maana tukaona ni vyema kufanya mafunzo haya kwa viongozi wa dini kwani ni wadau muhimu wakuhamasisha na kutoa elimu ya masuala ya lishe kwa jamii hivyo Sisi kama Jiji la Dar es Salaam tutaendelea kushirikiana viongozi wa dini kufanikisha adhima hiyo kwa kuendelea kutoa elimu na hamasa ya masuala ya Lishe kupitia majukwaa ya dini katika jamii”.Ameeleza Dkt. Mlay.
Sambmba na hilo, amewataka Wananchi kuhakikisha wanakula mlo kamili wenye virutubisho vyote muhimu vya makundi ya chakula kwa ajili ya ukuaji wa binadamu ikiwemo protini, wanga, vitamini, madini, mboga mboga, matunda na maji ili kuimarisha afya zao na kujikinga na magonjwa yasiyoambukizwa kama kisukari na presha.
Kwa upande wake Afisa Lishe Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam Bi. Flora Mgimba ameeleza kuwa lengo la mafunzo haya ni kuhamasisha na kuwajengea uwezo viongozi wa dini juu ya masuala ya lishe yanayoikabili jamii kwani viongozi wa dini wanaifikia jamii kwa ukaribu zaidi.
“Sisi kama Halmashauri tumeona viongozi wa dini ni wadau pekee wanaoweza kutumia majukwaa yao katika kuelimisha jamii juu ya masuala ya lishe kwani suala ya lishe ni mtambuka katika nchi yetu hivyo kwa kuandaa mafunzo haya tunaamini viongozi hawa wataendelea kuhamasisha na kutoa elimu ya Lishe kwa jamii ambayo italeta matokeo chanya katika kuboresha Afya za wananchi pamoja na kupambana na changamoto ya utapiamlo ikiwemo lishe pungufu, upungufu wa vitamini,madini na lishe ya kuzidi hii ikiwa ni kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhakikisha inapambana na lishe duni kwa jamii ili kutengeneza kizazi chenye Afya bora kwa maendeleo endelevu ya Taifa letu”. Amehimiza Bi. Flora
Akitoa Shukrani kwa niaba ya washiriki wengine Mchungaji kutoka Kanisa la Menonite Tanzania Rev. Suleiman Orwa amesema ili kuongoza waumini katika ibada ni lazima kuongoza waumini wenye Afya bora na kuahidi kuutumia muongozo huo na mafunzo hayo katika kuhamasisha na kuelimisha jamii kuhusu lishe bora ili kufikia lengo la Pamoja la kuwa na jamii yenye Afya bora. "Kwenye maandiko ya Mungu biblia inasema miili yetu ni hekalu la Roho Mtakatifu hivyo miili yetu ni sehemu ya kufanyia ibada hivyo inahitajika kuwa ni miili yenye afya nzuri, akili yenye ubunifu mzuri kwa ajili ya huduma za kiroho, hivyo baada ya kupitishwa kwenye mafunzo haya tunaahidi kwenda kuwafundisha waumini wetu”
Aidha, katika mafunzo hayo viongozi hao wameelezwa kuhusu ugonjwa wa MPOX ambao hunasababishwa na virusi aina ya Monkeypox unaopatikana kwa jamii ya wanyama ambao ni nyani, sokwe na Ngedere ambapo maambukizi haya huambukizwa endapo mtu atang’atwa na moja ya myama huyo au kugusana na mtu mwenye ugonjwa huo hivyo wananchi kuendeleea kupewa tahadhari ya namna ya kujikinga na ugonjwa huo kwa kunawa mikono kwa maji tiririka, kuepuka kugusana kwa kupeana mikono au kukumbatiana, kuvaa barakoa pamoja na kuwahi kituo cha huduma za afya pindi wanapoona dalili za MPOX huku viongozi wa dini wakihimizwa kuendelea kutoa elimu kwa jamii ya namna ya kujikinga na ugonjwa huo wa MPOX kwa kuzingatia kanuni za afya ikiwemo kula mlo kamili na kufanya mazoezi ili kuongeza kinga za mwili kwa kupambana na magonjwa ya mlipuko kama hayo.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.