Katika kutekeleza mkataba wa lishe ngazi ya Wilaya, Halmashauri ya Jiji la DSM leo Mei 17, 2024 imefanya halfa fupi ya kukabidhi bajaji 5 zenye thamani ya shilingi milioni arobaini na tano (45,000,000) ambazo zitasaidia kufanya ufuatiliaji wa lishe, mazingira na afya kwa mama na mtoto pamoja na vibao vya kupimia urefu kwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano vyenye thamani ya milioni ishirini na mbili (22,000,000).
Akiongea wakati wa kukabidhi vitendea kazi hivyo, Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe Edward Mpogolo amesema “Kipekee napenda kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuboresha huduma za afya kwa wananchi, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa miundombinu ya Afya kwani ametoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa vituo vikubwa viwili vya afya ambavyo ni Mchikichini chenye thamani ya Bilioni Tano na Kituo cha Afya Mzinga chenye thamani ya Bilioni 2.7, Lengo likiwa ni wananchi wapate huduma za Afya katika maeneo ya karibu."
Sambamba na hilo, Mhe Mpogolo amesema kuwa ili uweze kutoa huduma na Elimu ya Afya na lishe katika maeneo mbalimbali ni lazima uwe na vitendea kazi ambavyo ni usafiri hivyo Halmashauri ya Jiji la DSM kupitia kwa Mkurugenzi wametenga fedha kwaajili ya kununua bajaji 18 ili ziweze kurahisisha utoaji wa Elimu hasa katika masuala ya lishe kwa wananchi wa Wilaya ya Ilala.
Aidha, Mkurugenzi wa jiji la DSM Jomaary Satura amesema “Taifa letu ili tuwe na maendeleo inatupasa kusimamia rasilimali watu kwa kutoa Elimu ya lishe katika Jamii hasa kwa watoto tangu akiwa tumboni hadi kufikia umri wa miaka 5 ili kuepuka udumavu wa akili, hivyo tunagawa bajaji na vibao hivi kwa wataalamu wa lishe ili waweze kumsimamia mtanzania kuimarisha Afya yake na awe na uwiano sawa wa akili (maarifa) na umri wake."
Awali akisoma taarifa ya uzinduzi wa bajaji na vibao vya kupima urefu kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano, Mganga Mkuu wa Jiji la DSM Dkt. Zaituni Hamza amemshukuru Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi kwa kuendelea kutoa fedha kwaajili ya afua za lishe na kuahidi kuendelea kutekeleza majukumu kwa weledi.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.