Jiji la Dar es Salaam leo Desemba 17 limepokea ujumbe wa Viongozi na Watendaji kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Tabora waliofanya ziara ya kujifunza mbinu mbalimbali za ukusanyaji wa mapato, usafi wa mazingira na Usimamizi wa Miradi pamoja na kutembelea Soko la Kimataifa la Samaki Feri kujifunza uendeshaji wa masoko.
Ujumbe huo uliongozwa na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Tabora Mhe. Ramadhani Kapela, ambaye amewashukuru viongozi na watendaji wa Jiji la Dar es Salaam kwa mapokezi mazuri na kukubali kuwapatia mafunzo hayo na kuwapongeza kwa ukusanyaji wa mapato.
Akiongea wakati wa kufunga mafunzo na ziara hiyo kwa niaba ya Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha, Diwani wa Kata ya Ukonga Mhe. Ramadhani Bendera amesema “Nachukua nafasi hii kuwakaribisha katika Jiji la Dar es Salaam na tumefarijika kupokea ugeni huu mkubwa kutoka Rungwe hii inatupa uwezo wa kubadilishana uzoefu, sisi tuwape yetu lakini pia tupokee kutoka kwenu.”
Naye Mkurugenzi wa Manispaa ya Tabora Elias Kayandabila amesema kuwa wamejifunza mambo mengi mazuri ambayo hapo awali walikuwa hawayafahamu hivyo kwa namna moja au nyingine yatabadilisha utendaji wao wa kazi na kuleta matokeo chanya katika Halmashauri yao.
“Tumejifunza mambo mengi ambayo tulikuwa hatuyafahamu hapo awali. Tumejifunza mbinu hasa uanzishwaji wa kanda katika kusimamia na kukusanya mapato na usafi wa mazingira . Nina imani haya yote tuliyojifunza tukiyaweka kwenye utekelezaji tutakuwa tumepiga hatua kubwa.” amesema Mkurugenzi Kayandabila.
Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imekuwa ikipokea wageni mara kwa mara kutoka ndani na nje ya nchi wanaokuja kujifunza namna inavyotekeleza majukumu yake na kupata mafanikio makubwa katika nyanja mbalimbali.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.