Imeelezwa kuwa Halmashauri ya Jiji la Dar es salaam imetenga takriban Sh. 853 milioni ili kuwezesha vikundi vya vijana, wanawake na watu wenye walemavu katika bajeti ya mwaka 2019/2020.
Hayo yameelezwa leo tarehe 20 Juni, 2019 jijini Dar es Salaam na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Herman Msuha katika ziara ambayo wameifanya kwenye viwanda vidogo vidogo vilivyopo Mwananyamala ikiwa ni muendelezo wa Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma.
Msuha amesema kwa mujibu wa maelekezo ya Serikali kila Mamlaka za Serikali za Mitaa nchini, zinatakiwa zitenge 10% ya mapato yake ya ndani ili kuweza kuwawezesha vijana, wanawake na watu ulemavu na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imetekeleza hilo kwa ujenzi wa miundombinu, majengo na maeneo ya huduma kwa ajili ya wajasiriamali wadogo kwa kushirikiana na Shirika la Viwanda Vidogo Vidogo (SIDO).
Aliendelea kueleza kwamba lengo la ujenzi wa viwanda vidogo vidogo ni kuwafikishia huduma muhimu wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kwa pamoja ili wajikwamue kiuchumi, kujiongeza kipato na kupunguza tatizo la ajira hasa kwa vijana, kina mama na watu wenye ulemavu kwa kuwarasimisha wajasiriamali hawa wadogo ambao wengi hawako rasmi kwa kukosa sehemu za kufanyia kazi.
Aidha ameeleza kuwa Jiji limekwisha sajili vikundi 300 ambapo 15 vinapatikana eneo la Mwananyamala huku akisema katika mwaka ujao wa fedha watajenga kituo cha mafunzo kwa wajasiriamali pamoja na kuongeza miundombinu ya viwanda vidogo vidogo viwili jambo ambalo litakalosaidia idadi ya wanufaika kuongezeka.
Kwa upande wao wazalishaji wa bidhaa mbalimbali waliopo katika viwanda hivyo vidogo wametoa pongezi kwa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa kuwapatia mikopo pamoja na kuwajengea uwezo kupitia mafunzo ambayo yanasaidia kuboresha zaidi uzalishaji na biashara zao na wamwaomba Watanzania kujijengea tabia ya kutumia bidhaa zinazozalishwa hapa nchini.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.