Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa kushirikiana na Wadau mbalimbali leo tarehe 31 Oktoba, 2019 katika ukumbi wa Karimjee wamezindua Mpango Mkakati wa udhibiti na usimamizi wa maeneo ya ukijani jijini Dar es Salaam.
Akizindua Mwongozo huo kwa niaba ya Mkurugenzi wa Jiji, Mkuu wa Kitengo cha Itifaki na Uhusiano wa Umma wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Gaston Makwembe alieleza kwamba Jiji la Dar es Salaam na wadau mbalimbali kwa pamoja wanaendelea na jitihada za kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabia nchi jijini zikiwemo mafuriko, ongezeko la hali ya joto na kupitia Mwongozo huu Mamlaka za Serikali za Mitaa jijini Dar es Salaam na wadau mbalimbali watautumia kama nyenzo katika kukabiliana na changamoto kuu za Miji duniani na kuhakikisha kwamba wakazi wote wa Dar es Salaam wanaishi katika mazingira salama, wanafurahia maisha mazuri katika jamii zao na wanaweza kuwa na maisha endelevu.
“Jiji la Dar es Salaam ni moja ya majiji yanayokua kwa kasi zaidi duniani na bado lina maeneo mengi ya asili ambayo yana faida na yatoa huduma muhimu kwa Jiji na wakazi wake ikiwemo uwepo wa Pwani na fukwe zenye madhari nzuri, mito na vijito, mikoko, misitu na aina mbalimbali za wanyama pori”, aliendelea kueleza Makwembe.
Aidha, amesema kuwa na Mwongozo thabiti, rasilimali hizi zinatakiwa zilindwe, zirejeshwe, zikuzwe na hata kuongezwa ili kuendelea kutoa faida mbalimbali zikiwemo vyanzo vya maji safi na salama, chakula, ajira, uratibu wa hali joto la Jiji, kupunguza uchafuzi wa hali ya hewa, kukinga na majanga ya asili, fursa za utalii, maeneo ya starehe na mapumziko na kujisikia fahari juu ya maeneo yetu.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.