Na: Doina Mwambagi
Kamati ya Fedha na Utawala ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam Leo februari 26, 2025, imefanya ziara ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika jiji hilo kwa kipindi cha robo ya pili ya mwaka wa fedha 2024/2025 (Oktoba – Desemba 2024).
Katika ziara hiyo, kamati imetembelea miradi miwili muhimu ya sekta ya afya, ambayo ni ujenzi wa ghorofa ya Kituo cha Afya Mchikichini chenye thamani ya Bilioni 5.2 na jengo la Mama na Mtoto katika Kituo cha Afya Mnazi Mmoja lenye thamani ya zaidi ya milioni 295.
Akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Kamati, Mheshimiwa Nyansika Getama, ambaye ni Mwenyekiti wa kamati ya Mipango miji na Mazingira amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuipatia Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam fedha za ujenzi wa vituo hivyo vya Afya .
“Ujenzi wa kituo cha afya cha mchikichini na jengo la mama na mtoto utasaidia kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi, na kuhakikisha matibabu bora na kwa wakati, na kupunguza changamoto zilizokuwepo awali. Hivyo tuna kila sababu za kumshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuipatia Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam fedha za ujenzi huu muhimu ambao utaleta mabadiliko chanya kwa jamii yetu.” Amesisitiza Mhe. Getama
Aidha, kamati imeagiza wahandisi wa Halmashauri kuhakikisha miradi inatekelezwa na inakamilika kwa wakati uliopangwa. Huku wakiwataka wakandarasi kufanya kazi kwa viwango vya juu ili kuhakikisha miradi hiyo inadumu kwa muda mrefu na kuwanufaisha wananchi.
Ziara hiyo ni sehemu ya jitihada za Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam katika kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa ufanisi na kuleta manufaa kwa jamii.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.