Kamati ya Lishe Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam leo Septemba 19, 2023 wamefanya kikao cha kawaida cha Kujadili taarifa za utekelezaji wa Kazi za Lishe kwa kipindi cha robo ya nne kuanzia Aprili hadi Juni 2023.
Akifungua kikao hicho Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam Bi. Tabu Shaibu amesema kuwa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam inatekeleza maagizo ya upatikanaji wa lishe kwa vitendo kwani Serikali ya Tanzania imedhamiria kuendelea kulipa umuhimu wa kipekee suala la lishe bora nchini kwani ni suala mtambuka hivyo kamati ya lishe ihakikisha inajikita zaidi kuhamasisha na kutoa elimu kuhusu mlo kamili na namna ya uandaaji wa mlo huo huku akiwakumbusha wajumbe wote wa kamati ya lishe kuhakikisha mambo waliyokubaliana katika kikao hicho yanafanyiwa kazi ili kufikia malengo waliojiwekea.
Katika kikao hicho Divisheni mbali mbali ziliwasiliisha taarifa za utekelezaji wa kazi za lishe kwa kipindi cha robo ya nne ambapo baada ya taarifa hizo Kamati iliweza kujadili na kutoa maelekezo kwa Divisheni ya Elimu Sekondari kuhamasisha zaidi suala la lishe kwa wanafunzi kwani inaonekana Shule nyingi za Sekondari na Msingi wanafunzi hawapati mlo kamili.
Vilevile kwa upande wa Divisheni ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Afisa Kilimo Bi. Fatuma Mahanaka amesema suala la kutoa elimu kwa wakulima na wafugaji limetekelezwa kwa kutoa ushauri na elimu ikiwa ni pamoja na kuwasisitiza kuhifadhi vyakula na kuweka akiba ya mifugo kwa matumizi ya baadae huku akiahidi kuendelea kushirikiana na Idara za Elimu Sekondari naMsingi kuendelea kutoa elimu ya lishe shuleni hususani kuwafundisha wanafunzi namna ya kulima kilimo cha uyoga kwani uyoga ni zao zuri kwa kuboresha Afya ya akili na ya mwili pia.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam Dkt. Zaituni Hamza ameeleza kuwa “Afua ya Lishe inasimamiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan tusimuangushe tusimame nae bega kwa bega kuhakikisha masuala ya elimu na utekelezaji wa afua za lishe kwa wanafunzi na jamii kwa ujumla hivyo niwasihi sana kuimarisha masuala ya lishe kwenye jamii zetu kwani lishe imekua ni changamoto na nitoe wito kwa kila mjumbe aifanye ajenda na kutembea nayo kuelimisha wananchi kuhusu mlo kamili na aina ya vyakula vinavyostahili kuliwa hivyo Divisheni ya Kilimo mhakikishe mnatoa mchango wenu wa kusimamia namna ya bora ustawishaji wa mazao kwa afya bora.”
Aidha katika kikao hicho wajumbe walikubaliana katika kuongeza jitihada zaidi katika kuandaa programu za kuhamasisha na kutoa elimu za mara kwa mara kwa wananchi juu ya masuala ya lishe hususani mashuleni na kwa mama lishe ili kuboresha Afya za wananchi kwa maendeleo ya Nchi.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.