Jumla ya Waheshimiwa Madiwani 21 kati ya 26 wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam leo Desemba 23, 2020 wameapishwa na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Sokoine Drive Mheshimiwa Anipha A. Mwingira katika ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam.
Akizungumza mara baada ya kuapishwa na kufungua Mkutano kwa kwanza wa Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Mstahiki Meya Omary Matulanga amewataka Madiwani wenzake kufanya kazi kwa ushirikiano kwa ajili ya kuendeleza Jiji la Dar es Salaam.
Aidha, Matulanga amesema Jiji la Dar es Salaam ni Jiji kubwa la kibiashara hivyo ni wajibu wa kila Diwani kuhakikisha anafanya kazi kwa ubunifu, weledi na kwa kuzingatia taratibu, miongozo na sheria ya maadili ya viongozi wa umma.
Katika hatua nyingine, Matulanga ametangaza Kamati za Kudumu za Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam na majina ya Waheshiwa Madiwani ambao ni Wajumbe wa Kamati hizo ambapo pia walipata fursa ya kuwachagua Wenyeviti wa Kamati.
Waheshimiwa Madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam pia walipata nafasi ya kupokea taarifa ya utekelezaji wa shughuli za kila siku na za miradi ya maendeleo iliyotekelezwa katika kipindi ambacho Menejimenti ya Halmashauri ya Jiji ilipokasimiwa madaraka ya Baraza la Madiwani.
Hata hivyo, Baraza hilo limeshindwa kufanya uchaguzi wa Naibu Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kutokana na kutokamilika kwa mchakato wa uteuzi wa jina la mgombea nafasi hiyo ndani ya Chama kutokamilika.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.