Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imeboresha mfumo wa ukusanyaji wa ada za maegesho kwa kuunganisha na mfumo wa Tausi, hatua inayolenga kurahisisha huduma kwa wananchi. Hatua hii inakuja baada ya changamoto zilizojitokeza katika mfumo wa awali wa TERMIS ambao haukufanikisha malengo kikamilifu.
Akizungumza na waandishi wa habari leo tarehe 7 Februari 2024 kuhusu maboresho haya, Kaimu Mkurugenzi wa Jiji, Tabu Shaibu amesema kuwa mfumo mpya wa Tausi utawezesha wananchi kulipia maegesho kwa njia ya kidigitali kupitia simu zao, huku ukihakikisha uwazi katika makusanyo ya mapato.
Bi Tabu amesema Halmashauri ya Jiji la Dar es salaam imefanya maboresho haya yanalenga kupunguza mianya ya upotevu wa mapato na kuimarisha usimamizi wa maegesho mijini.
"Mfumo wa Tausi unasaidia kuratibu taarifa kwa usahihi, na kurahisisha usimamizi wa maegesho na kuhakikisha huduma bora kwa wananchi" amesisitiza Bi Tabu.
Aidha, Kaimu Mkurugenzi huyo amewataka wakazi wa jiji la Dar es Salaam kutumia mfumo huu mpya kwa ufanisi ili kufanikisha lengo la kuboresha huduma za maegesho Huku akiwaahidi kuendelea kufanya maboresho ya mifumo ya kidigitali ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za umma.
Kwa Upande wake Meneja wa Maegesho wa Halmshauri ya Jiji la Dar es Salaam Bi Neema Ngavatula ameeleza faida mbalimbali za Mfumo huo ikiwemo Mtumiaji kupata kifurushi Cha masuala ya maegesho, eneo alilopaki na kupata huduma ya kupata Maombi ya maegesho maalumu.
Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam itaendelea kusimamia na kufuatilia utekelezaji wa mfumo huu ili kuhakikisha unaleta manufaa yanayotarajiwa kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.