MSTAHIKI Meya wa Jiji la Dar es Salaam Isaya Mwita jana aliwafuturisha wakazi wa Jiji la Dar es Salaam zaidi ya 600 kutoka sehemu mbalimbali jijini hapa nakutumia nafasi hiyo kuwatakia waumini wote wa dini ya Kiislam heri ya kumalizia Ibada ya kufunga Mwezi Mtukufu wa Ramadhani sambamba na kuingia kwenye sikukuu ya Idd.
Aidha Mashehe wa Jiji la Dar es Salaam waliohudhuria hafla hiyo jana walimpongeza Meya Mwita kwa kuandaa futari hiyo na kusema kuwa ni jambo la heri kwao na hivyo wataendelea kumuunga mkono katika shughuli zake za kuwaongoza wananchi kwa ajili ya kuwaletea maendeleo.
Hafla hiyo ambayo ilihudhuriwa na Kadhi Mkuu wa Mkoa, Mashehe wa Jiji la Dar es Salaam, viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa, makundi mbalimbali ya kijamii, ilifanyika katika viwanja vya Karimjee jijini hapa.
Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa futari hiyo jana Meya Mwita alisema kuwa kupitia mfungo wa Ramadhani wakazi wa Jiji na watanzania wote kwa ujumla wanapaswa kuzidisha hali ya unyenyekevu, ucha Mungu ili kutenda mambo yaliyo mema na hivyo kusherehekea sikukuu ya Idd kwa hali ya utulivu.
Meya Mwita alifafanua kuwa kupitia hafla hiyo imekuwa ni fursa ya kipekee kujumuika pamoja na wananchi wa jijini hapa kuzungumza mambo mbalimbali ya maendeleo na kutumia nafasi hiyo kuwaalika kwenye ofisi za Jiji ili aweze kusikiliza kero zinazo wakabili na kuzipatia ufumbuzi wa haraka.
“Nimefarijika sana leo, kujumuika pamoja kwenye tukio hili muhimu ambalo hutokea kila mwaka, lengo la kuwa na hafla hili, ni kuungana na waumini wote wa dini ya Kiislam wa jijjni hapa ambao wako katika mwezi mtukufu wa Ramadhani "
"Lakini pia hata wale ambao hawapo kwenye mfungo huu, kupitia hadhara hii tunaweza kukutana na wakazi wengi zaidi na kubadilishana mawazo”, alisema Meya Mwita. Jiji la Dar es Salaam lina wakazi wengi sana, ambapo huwezi kusema kwamba leo utakwenda kukaa na kila mmoja, lakini yapo matukio ambayo yanatukutanisha kama wanafamilia wa jiji la Dar es Salaam, na hii kwangu ndio faraja zaidi kwani tunakutana kwenye matukio ya kiimani, na siyo ya kisiasa.
Kwa upande wake Shehe wa Wilaya ya Ilala Adam Mwinyipingu alimpongeza Meya Mwita kwa kuandaa hafla hiyo iliyomkutanisha na baadhi ya wananchi ambao walishiriki futari hiyo. Shehe Mwinyipingu alisema kuwa jambo hilo ni la heri kwa waumini wote wa kiislam na wananchi wote waliohudhuria hafla hiyo ya futari.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Temeke, Abdallah Mtolea pamoja na mambo mengine alimpongeza meya Mwita kwa kuandaa hafla hiyo, na kusema kuwa imesaidia kuwakutanisha na wananchi wao ambao si rahisi kukutana nao mara kwa mara kutokana na shughuli zao.
“Kwa siku ya leo nimeifurahia nimeweza kujumuika na viongozi mbalimbali wa dini, vyama vya kisiasa, na wananchi wa Jiji hili ambao tunashindwa kukutana mara kwa mara kutokana na shughuli mbalimbali ambazo wametupatia wananchi ili kuwatumikia.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.