Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Mussa Azzan Zungu amekabidhi zawadi ya mipira 180 kwa shule 36 za Msingi na Sekondari zilizopo Jimbo la ilala zilizotolewa na wadhamini kutoka Shirika la Lions International kwa kushirikiana na Nazneen Material Holding Limited.
Mhe. Zungu amekabidhi zawadi hizo katika Maadhimisho ya Siku ya Huduma kwa Jamii Duniani yaliyofanyika katika shule ya Msingi Upanga Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika maadhimisho hayo Mhe. Zungu amesema "Kitendo cha leo kilichofanywa na wadhamini hawa cha kugawa mipira mmewapa furaha watoto wetu maana mwili ukiwa na afya hata ubongo unakua na afya, pia nawapongeza kwa kuunga mkono juhudi za Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika suala la michezo, na kwa zawadi hizi mtaibua wachezaji wengi wapya wa timu zetu ya Taifa."
Kwa upande mratibu wa Shirika la Lions Clubs International Bi. Nimira H. Ganji amemshukuru Mhe. Zungu kwa kukubali kushirikiana nao katika halfa ya maadhimisho hayo na kueleza kuwa wameamua kutoa mipira kwa watoto wa Shule za Msingi na Sekondari kwa sababu michezo ni chachu ya maendeleo katika masomo kwa wanafunzi kwani mtoto anakua imara kiakili, kimwili na kiafya.
Aidha, Mkurugenzi wa Nazneen Material Holding Limited Ndg. Mohamed Jawad Kassam ameeleza kuwa vipaji huanzia ngazi ya chini hivyo wametoa zawadi ya mipira ili kuibua vipaji vya mipira kwa watoto ili kuweza kupata wachezaji wazuri wa mpira wa miguu kwa wanawake na wanaume.
Akifunga halfa hiyo Diwani wa Kata ya Upanga Mashariki Mhe. Sultan Ahmed Salim amesema "Nakushukuru sana Mhe. Naibu Spika kwa kushirikiana nasi katika mambo mbalimbali ya kijamii. Pia nawashukuru wadhamini kwa kuchagua Kata yetu kufanyia maadhimisho ya Huduma kwa Jamii Duniani."
Maadhimisho ya Siku ya Jamii Duniani huadhimishwa kila Oktoba 13.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.