Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Mhe.Albert Chalamila leo tarehe 30 Mei, 2023 amefanya kikao maalum na Viongozi pamoja na Watumishi wa ngazi ya Wilaya na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa lengo la kujitambulisha rasmi la kuomba ushirikiano katika utendaji kazi.
Kikao hicho kilichofanyika katika Ukumbi wa mikutano wa Karimjee kilihudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe.Edward Mpogolo, Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya, Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Naibu Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Madiwani, Watendaji wa Kata na Mitaa, Wakuu wa Divisheni na Vitengo na watumishi wa Jiji la Dar es Salaam kutoka kada mbalimbali.
Akiongea na watendaji hao Mhe.Chalamila amewaomba wampe ushirikiano wa kutosha katika kuwatumikia wananchi ili kufanikisha malengo makubwa ya Serikali ya Awamu ya Sita ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Aidha amewasisitiza kupenda kufanya kazi kwa uwazi na kuepuka mambo ya rushwa na kuonea raia kwa kutumia madaraka waliyonayo kuwanyanyasa na kuwanyima haki zao, Amesema “Naomba muwe watu wa kusimamia haki kila wakati, sipendi watendaji ambao wanatumia ujanja ujanja katika kutekeleza majukumu yao. Fanyeni kazi kwa uwazi epukeni rushwa kwa kuwa rushwa ni adui wa maendeleo.”
Mbali na hilo Mhe. Chalamila amewataka watumishi kudumisha ushirikiano baina yao ili kutimiza majukumu yao ipasavyo kwa sababu katika utumishi kila mmoja anafanya kazi kwa kumtegemea mwenzake kwa maslahi mapana ya jamii na nchi yetu kwa ujumla.
Vilevile amewaomba watumishi hao kuendelea kusimamia kwa uadilifu miradi mbalimbali ya maendeleo inayoendelea kutekelezwa katika Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ili Mhe. Rais aweze kuwapatia tena fedha za kuendeleza na kuanzisha miradi mingine mikubwa ya maendeleo. Pia amewataka kusuluhisha kwa wakati migogoro mbalimbali iliyopo katika jamii hasa migogoro ya ardhi kwani baadhi ya migogoro inasababishwa na watendaji wenyewe na kuwaomba waepuke kuwa sehemu ya migogoro iliyopo katika jamii.
Mhe.Chalamila pia amefurahishwa na kampeni iliyokuwepo ya kuwapanga wafanyabiashara ndogondogo katika maeneo rasmi ili kuhakikisha Jiji linakuwa katika hali ya usafi kila wakati na kutoa rai kwa watumishi na viongozi wote kuendelea kuisimamia kampeni hiyo kwa vitendo, na kwamba yeye anaiunga mkono na ataendelea kuisimamia kwa uwekaji wa taa za barabarani ili kupunguza Uhalifu uliokuwepo awali. Vilevile ameahidi kuwa katika uongozi wake hapa Dar es Salaam, atahakikisha mwarobaini wa uchakataji taka ngumu unapatikana.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.