Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Ilala Ndg. Sosthenes Kibwengo ametoa rai kwa walimu wa shule za msingi kuanzisha klabu za kupinga rushwa katika shule zao ili kuwawezesha vijana kutambua nafasi na wajibu wao katika mapambano dhidi ya rushwa na kuwafanya washiriki ipasavyo katika kuzuia na kupambana na rushwa.
Ndg. Kibwengo ameyasema hayo wakati wa mafunzo kwa walimu wa shule za msingi za Serikali na binafsi yaliyofanyika leo tarehe 16 Oktoba, 2023 katika Shule ya Msingi Kisutu.
Aidha, ameongeza kuwa wameamua kutoa mafunzo ya kuzuia na kupambana na rushwa kwa walimu kwani wao ndio daraja ambalo vijana wanapaswa kulipanda ili nchi ifikie malengo iliyojiwekea kwa sababu Tanzania ya leo na kesho inahitaji vijana waadilifu, wazalendo, wapenda haki na wale wanaoamini kuwa kufanya kazi ndio njia pekee ya mafanikio.
"TAKUKURU tumeamua kuwekeza kwa vijana kwa wao ndio taifa la kesho. Kijana anayetumia madawa ya kulevya na asiyejua madhara ya rushwa hawezi kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya familia na ujenzi wa taifa kwa ujumla." Amesema Ndg. Kibwengo
Naye mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo Mwl. Sophia Daniel wa shule ya Msingi Kiwalani amewashukuru TAKUKURU Mkoa wa Ilala kwa kuandaa mafunzo hayo kwao na kusema kuwa mafunzo watakayoyapata yatawasaidia kuwawezesha wanafunzi katika kupinga na kupambana na rushwa pamoja na madawa ya kulevya na kutoa wito kwa walimu wenzake ambao ni walezi wa wanafunzi hao wawapo shuleni kuwa na mikakati endelevu katika klabu walizozianzisha ili watoto waendelee kukua katika maadili mema wakitambua madhara yatokanayo na rushwa na madawa ya kulevya kwa ustawi bora wa nchi.
TAKUKURU kupitia Idara yake ya Elimu kwa Umma imekuwa na utaratibu wa kutumia mbinu mbalimbali kuwaelimisha na kuwashirikisha wanajamii wa makundi mbalimbali ikiwa ni pamoja na vijana walioko shuleni kwa kuanzisha Klabu mbalimbali za kupinga na kupambana na rushwa na dawa za kulevya kwa lengo la kuwajenga vijana kimaadili kwa kuwafanya watambue madhara ya rushwa na kujenga jamii ya watu waadilifu.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.