Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Edward Mpogolo amewataka Vijana kuachana na matumizi ya dawa za kulevya na badala yake waungane katika kufanya shughuli halali za kiuchumi ili wajiletee maendeleo katika ngazi ya familia, jamii na hata Taifa.
Mhe. Mpogolo ametoa wito huo leo Julai 05 2024, wakati wa akifunga Kongamano la Vijana la Kapinga Matumizi ya Dawa za Kulevya lililofanyika katika viwanja vya Usikate Tamaa vilivyopo Vingunguti Jijini Dar es Salaam sambamba na kaulimbiu isemayo ‘WEKEZA KWENYE KINGA NA TIBA DHIDI YA DAWA ZA KULEVYA” ambayo inalenga Serikali, wadau, vijana na wananchi kwa ujumla kuwa na dhamiri ya dhati katika kuwekeza kwenye kinga na tiba ilikupunguza au kuondoa kabisa tatizo la matumizi ya dawa za kulevya hasa kwa vijana kwani kinga na tiba ni uhakika wa ushindi wa mapambano dhidi ya dawa za kulevya.
Akizungumza na vijana pamoja na Wananchi waliohudhuria katika Kongamano hilo Mhe. Mpogolo amesema “Kufuatia wimbi la vijana kuingia katika matumizi ya madawa ya kulevya pamoja na kupata madhara mbalimbali ya kiafya, Serikali imejikita katika kutoa elimu ili jamii ifahamu hivyo Kwa juhudi zinazoendelea za kupambana na matumizi ya madawa ya kulevya, nitoe pongezi na shukrani za dhati kwa kazi kubwa inayofanywa na Uongozi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa kushirikiana na Wadau mbalimbali ikiwemo MDH, DEH pamoja na Peer to Peer Group katika kuchochea, kuhamasisha na kuratibu shughuli zote za mapambano dhidi ya matumizi ya dawa za kulevya na kuwekeza kwenye kinga na tiba dhidi ya dawa za kulevya. Pia niwasihi vijana wengine ambao hamjaingia kwenye madawa msishawishike kuingia huko na ambao mshaathirika na madawa muendelee kutumia dawa za kuwakinga ili msiathirike zaidi.”
Sambamba na hilo Mhe. Mpogolo amewataka Vijana kuwa na Maadili mema pomoja na kujiepusha na makundi ya ushawishi ili kulinda afya zao na nguvu kazi ya taifa huku akiwataka wajikite zaidi na Shughuli za kimaendeleo pamoja na kuwasisitiza vijana hao kuwa mabalozi wazuri katika kuwaelimisha wale wote ambao hawakupata nafasi ya kushiriki katika kongamano hilo kuhusu athari na madhara ya matumizii ya dawa za kulevya kwa ustawi wa jamii na Taifa kwa ujumla.
“Tunawahimiza kuacha kujihusisha na shughuli zinazokinzana na sheria, taratibu na kanuni za nchi yetu badala yake vijana tutumie mazingira wezeshi tuliyowekewa na Serikali kuongeza ufanisi katika kukuza taaluma, uchumi, elimu na biashara ili kufikia malengo yetu hivyo napenda kuwahakikishia kuwa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya tutaendelea kushirikiana na wadau wote wa vijana kwa kuwawekea mazingira rafiki ili muweze kutekeleza majukumu yenu ipasavyo.” Amesisitiza Mhe. Mpogolo
Katika hatua nyingine Mhe. Mpogolo amewasihi vijana na wananchi wa Wilaya ya Ilala kuhakikisha wanashiriki kikamilifu katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Oktoba 2024 huku akiwataka kujitokeza kwa wingi katika kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura pindi litakapofunguliwa.
Kwa upande wake Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam Mhe. Omary Kumbilamoto ameeleza kuwa ni mpango wa Serikali sasa katika kuhakikisha waraibu wote wa matumizi ya dawa za kulevya wanapewa huduma ya matibabu kuanzia ngazi ya zahanati, vituo vya afya na hospitali ambapo kwa sasa Serikali inaboresha kwanza huduma za afya kisha waanze kuratibu mpango huo hivyo amewasihi vijana wa Vingunguti kuhakikisha wana nitoke za kwa wingi kupata tiba na elimu.
Awali akisoma taarifa kwa Mkuu wa Wilaya Mratibu wa Shirika la utoaji elimu juu ya matumizi ya dawa za kulevya (NURGET) Bw. John Samson Busumabu ameeleza kuwa Taarifa ya Dawa za kulevya duniani inaonesha kuwa kumekuwa na ongezeko kubwa la biashara na matumizi ya Dawa za kulevya ambapo hali ya Dawa za Kulevya kwa mwaka 2021 ilionesha kuwa, takribani mtu 1 kati ya kila watu 17 wenye umri kati ya miaka 15 hadi 64 ulimwenguni walitumia Dawa za Kulevya. Katika kipindi cha mwaka uliopita, Idadi iliyokadiriwa ya watumiaji wa Dawa za Kulevya kwa miaka kumi imeongezeka kutoka milioni 240 mwaka 2011 hadi milioni 296 mwaka 2021 ambalo ni ongezeko la asilimia 23%. ambapo Katika kipindi hicho, Dawa za kulevya kama bangi, heroine, metamphetamine, cocaine pamoja na Dawa tiba zenye asili ya kulevya zilitumika. Mwaka 2020, inakadiriwa kuwa watu milioni 36 walitumia Dawa za kulevya jamii ya amphetamine (ATS), milioni 22 walitumia cocaine, na milioni 20 walitumia dawa aina ya “ecstasy” zilizopelekea madhara ya kiafya kwa watumiaji na jamii, kama vile ongezeko la maambukizi ya virusi vya UKIMWI, magonjwa ya akili na homa ya ini hivyo, jitihada mbalimbali zimeendelea kuchukuliwa ili kudhibiti uzalishaji, biashara na matumizi ya Dawa za Kulevya, ikiwa ni pamoja na utoaji wa tiba kwa watu wenye uraibu wa dawa hizo.
Aidha Bw. Busumabu ameeleza kuwa Halmashuri ya Jiji la Dar es Salaam imeweza kuungana na Wananchi wote Nchini na Duniani kote katika harakati za kudhibiti na kupambana na matumizi ya dawa za kulevya kwani Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam itaendelea kutoa elimu juu ya athari za matumizi ya dawa za kulevya ili kuzuia na kukinga watoto na vijana ambao hawajaingia kwenye matumizi ya dawa za kulevya na kuhakikisha kuwa hawaingii kwenye matumizi hayo huku wakiendelea kusaidiana na Serikali kupitia Mamlaka husika kuhakikisha linazuia uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa Dawa za kulevya nchini ili kuinusuru jamii dhidi ya Dawa za kulevya bila kusahau kuwatambua waraibu wa Dawa za kulevya na kuwaelimisha juu ya huduma za upunguzaji madhara ili kuchangia katika kuwasaidia waathirika wa dawa za kulevya kwa kuwaunganisha na huduma za afya kama kuwapeleka MAT kliniki kwa ajili ya kupata dawa ya maethadone ikiwa ni pamoja na kupata tiba za TB, Homa ya Ini na kupata dawa za ARV kwa walio na maambukizi ya Virusi vya UKIMWI.
Katika Kongamano hilo mada mbalimbali ziliweza kutolewa kwa vijana wapatao 1000 walioshiriki ikiwemo Madhara ya Matumizi ya Dawa za Kulevya ,Haki na Wajibu wa Kijana Kipindi cha Uchaguzi, Fursa za Kiuchumi kwa Vijana, Faida na Hasara ya mitandao ya Kidigitali, jinsi ya kujikinga na maambukizi dhidi ya VVU/UKIMWI pamoja na namna ya kuwa wazalendo na kujitolea kwa Vijana.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.