Ujumbe wa viongozi wa mji wa Kisumu nchini Kenya ukijumuisha Mameya, wahandisi, wajumbe wa bodi na wawakilishi wa bodaboda leo tarehe 9 Aprili, 2019 umefanya ziara ya siku tatu ya mafunzo kwa lengo la kujifunza na kubadilishana uzoefu katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo mradi wa mabasi ya mwendokasi pamoja na udhibiti wa taka ngumu jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Mwenyekiti wa Bodi ya Mji wa Kisumu, Elijah Adul Onyango mbele ya mwenyeji wake Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam Isaya Mwita Charles amesema Tanzania imepiga hatua katika mradi huo na imekuwa nchi ya kwanza ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kuwa na mradi huo wa kisasa wa usafiri wa umma.
“Mfumo huu wa usafiri ni muhimu sana kwa sababu utapunguza adha ya usafiri ikiwemo kupunguza muda watu wa Kisumu wanaoutumia wanapokwenda sehemu mbalimbali katika shughuli za kila siku mfano kazini na ndiyo maana tumekuja kujifunza na kubadilishana uzoefu jijini Dar es Salaam hususani changamoto na namna ya kukabiliana nazo kwa ajili ya utekelezaji wa mradi kwa ufanisi.”
Ujumbe huo pia umepata nafasi ya kusikia mawasilisho ya mikakati na jitihada mbalimbali zinazofanywa na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam pamoja na Manispaa zake katika udhibiti wa taka zinazozalishwa jijini zikiwemo uanzishwaji wa maeneo mapya ya madampo na vituo vya kukusanya na kusafirisha taka, urejelezaji wa taka kuwa mali pamoja na uhamasishaji kwa wadau mbalimbali wa Jiji la Dar es Salaam katika udhibiti wa taka kwa lengo la kuliweka Jiji katika mazingira safi na salama.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.