Mkuu Wa Wilaya anayehamia Wilaya ya Kwimba, Mkoani Mwanza Mhe. Ng'wilabuzu Ludigija leo tarehe 27 Januari, 2023 amefungua Mafunzo ya siku mbili kwa Viongozi wa Wafanyabiashara wa Soko la Machinga Complex katika Ukumbi wa Mikutano wa Silver uliopo Manzese Tiptop yenye lengo la kuimarisha mahusiano mazuri kati ya Wafanyabiashara na Serikali sambamba na kutatua migogoro ya Wafanyabiashara.
Mhe. Ludigija amesema mafunzo hayo yatapelekea Viongozi wa Soko hilo kuwa na uelewa wa pamoja katika kushughulikia changamoto zinazojitokeza eneo la kazi pia kutengeneza mazingira mazuri kwa Wafanyabiashara sambamba na kuimarisha uhusiano mzuri baina yao na Serikali.
“Kiongozi ni yule anayewaonesha njia anaowaongoza ili wafike salama,” Amesema Mhe. Ludigija
Aidha, ameongeza kuwa kuna haja Soko hilo kuwezeshwa ili kutoa huduma mbalimbali ambapo wananchi wataweza kupata huduma ndani ya Soko hilo kwa saa 24 'One Stop Centre'.
Naye, Meneja wa Soko hilo Bi. Stella Mgumia amemshukuru Mkuu wa Wilaya huyo kwa muda wote waliofanya naye kazi huku akisisitiza wapo tayari kuendelea kukaa na Wafanyabiashara na kuwawekea mazingira mazuri ili kukua kibiashara. Pia ameshukuru kwani mafunzo hayo yatazidi kuwajenga kimahusiano na kiuongozi na kutambua nafasi zao ambapo zitaenda kutatua changamoto kati ya Wafanyabiashara na Serikali. ”Mwisho wa siku mnaweza kumaliza Changamoto zenu kwa kukaa mezani” Amesema Bi. Stella wakati akiongea na wafanyabiashara hao
Akihitimisha, Mwenyekiti wa Wafanyabiashara Soko la Machinga Complex, Bwn. Bakari Mkupa amemwelezea Mkuu huyo Wa Wilaya kuwa Kiongozi Shujaa na mchapakazi akiongeza kuwa Wafanyabiashara wana imani na uongozi wa Mkuu mpya wa Wilaya kuendeleza yote yaliyokuwa yakifanywa na Mhe. Ludigija
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.