Wamiliki wa Vituo vya Afya Binafsi wa Mkoa wa Dar es Salaam wamepongezwa kwa kutoa huduma nzuri na Bora kwa wananchi wanaowazunguka. Pongezi hizo zimetolewa leo Desemba 6, 2023 wakati wa kikao kazi cha Wataalamu kutoka Wizara ya Afya, Bodi ya Hospitali Binafsi (PHAB), pamoja na Chama cha Wamiliki wa Vituo Binafsi vya Afya Tanzania (APHFTA).
Akizungumza kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mratibu wa Shughuli za UKIMWI Mkoa wa DSM Dkt. Ayoub Kibao amesema “Mkoa wa Dar es Salaam ndio unaoongoza kwa kuwa na asilimia kubwa ya vituo binafsi na wanufaika ni wananchi. Pia niwapongeze kwa utoaji mzuri wa huduma katika vituo vyenu na niwaombe muendelee kujali afya za watu na kufanya kazi kwa uweledi kwa kusimamia miiko ya kazi."
Awali akiongea katika kikao hicho, Msajili wa Hospitali Binafsi Dkt. Meshack Shimwela amesema ”Baraza la Hospitali binafsi nchini lilianzishwa mwaka 1970 likiwa na lengo la kutunza daftari la taarifa la vituo hivi na kuhakikisha zinatoa huduma kwa ubora wake ili kufikisha malengo ya Taifa. Hivyo niwapongeze wamiliki wote kwa kuendelea kutoa huduma bora na kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuboresha Sekta ya Afya Nchini."
Sambamba na hilo Dkt. Shimwela amesema hospitali binafsi zinasaidia katika kukuza mapato ya Taifa kwa kulipa kodi kusaidia kutatua changamoto ya ajira nchini, na pia zinatumika kama sehemu ya utalii (medical tourism).
Kikao hicho kinafanyika baada ya zoezi la Usimamizi Shirikishi Mkoa wa DSM na kililenga kuwapa mrejesho wamiliki wa Vituo vya Afya Binafsi wa yaliyobainika, lengo kuu likiwa ni kutoa huduma bora kwa Wananchi.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.