Kata ya Minazi Mirefu leo Januari 25, 2024 imefanya maadhimisho ya Siku ya Lshe yaliyofanyika katika Shule ya Sekondari Binti Mussa ikiwa ni muendelezo wa Sera ya Lishe Mashuleni iliyoanzishwa na Serikali Oktoba 2021.
Akiongea na wanafunzi, Mgeni rasmi katika Maadhimisho hayo Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa ya Mwale Ndg. Steven Ndawa amesema “Nawashukuru na kuwapongeza maafisa lishe kutoka katika Ofisi ya Mganga Mkuu pamoja na Afisa Mtendaji wa Kata ya Minazi Mirefu kwa kutuletea Elimu ya lishe katika shule yetu, Hakika elimu hii itawasaidia wanafunzi kuwaelimisha wazazi na walezi. Pia niwaombe elimu isiishie tu mashuleni bali mtuletee pia katika mitaa yetu ili Jamii iweze kuelewa umuhimu wa lishe bora."
Sambamba na hilo, Ndg. Ndawa amewaasa wanafunzi katika suala zima la usafi binafsi na mazingira ili kujikinga na magonjwa ya mlipuko ikiwemo kipindupindu na ugonjwa wa macho (red eyes).
Naye Afisa mtendaji wa Kata hiyo Ndg. Mohammed Bushiri amesema “Lengo la Serikali kuleta sera ya lishe mashuleni ni kuwapatia wanafunzi uelewa juu ta afya ya mwili na akili pia. Na naahidi kuisimamia sera hii katika shule zote zilizopo ndani ya Kata hii. Serikali inatoa Elimu bila malipo hivyo ni jukumu la wazazi kuchangia pesa ya chakula kwa wanafunzi kwa sababu ni mpango wa Kitaifa kuwa wanafunzi wapate chakula (mlo kamili) wawapo shuleni.”
Aidha, Kaimu Mratibu wa Lishe wa Jiji la DSM Bi. Neema Mwakasege amewaambia wanafunzi hao umuhimu wa lishe bora kuwa lishe bora iliyozingatia makundi sita ya vyakula inaweza kupambana na magonjwa mbalimbali kwa sababu mwili unakua na kinga imara zinazoweza kupambana na magonjwa.
"Lishe bora ni kula chakula cha kutosha na chakula chenye virutubisho vyote muhimu. Lishe bora husaidia mwili kukua vyema, kuujenga mwili lakini pia huimarisha kinga ya mwili ili kuweza kupigana na magonjwa. Ili lishe iwe bora ni muhimu iwe na mchanganyiko wa Makundi sita ya chakula ambayo ni protini, wanga, fati, mbogamboga, madini, matunda na maji kwa wingi hivyo tuhakikishe tunawapa watoto mlo kamili lengo likiwa ni kupunguza udumavu na kuongeza uelewa kwa watoto kwani lishe bora ndio msingi wa makuzi bora ya kimwili." Amesema Bi. Mwakasege.
Huu ni muendelezo wa utekelezaji wa mpango wa kutoa elimu ya lishe kwa wazazi, walezi na watoto katika Kata 36 na Mitaa 159 ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.