Katika kuhakikisha Mazingira yanakua safi, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kupitia Kitengo cha Maliasili na Uhifadhi wa Mazingira pamoja na Kitengo cha Usafishaji na Udhibiti wa Taka Ngumu kwa kushirikiana na Taasisi ya Eco Green Enviroment na BUDEO (BUGURUNI DEVELOPMENT ORGANISATION) leo Agosti 29, 2024 wametoa elimu kwa Wanafunzi wa Shule za Msingi na Sekondari Zanaki jinsi ya utenganishaji taka katika makundi matatu ambayo ni taka zitokanazo na mabaki ya vyakula, taka za plastiki pamoja na taka za karatasi lengo likiwa ni kuhakikisha wanafunzi hao wanafahamu umuhimu wa kutenganisha taka, ili kuboresha mazingira yanayowanzunguka na kuchangia maendeleo endelevu na yasiyo na uchafuzi.
Akitoa Elimu kwa Wanafunzi hao, Afisa Afya na Mazingira Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam Bi. Sarah Mwakijolo amesema kutenganisha taka kunahusiana na usafi wa mazingira ya watu na matumizi ya raslimali kwa kubana matumizi kwani kupitia usimamizi na mwongozo Jiji la Dar es Salaam linaweza kufanya watu washiriki zaidi kwenye kuendeleza desturi ya kutenganisha taka, kuboresha mazingira ya kuishi na kuchangia maendeleo endelevu yasiyo na uchafuzi huku akitoa wito kwa wanafunzi hao kuwa mabalozi wa kutunza mazingira kuanzia kwenye ngazi ya familia mpaka mashuleni kwa ustawi wa afya zao .
Sambamba na hilo Bi. Mwakijolo amewasisitiza wanafunzi hao kuwa mabalozi wa kuweka mazingira kwa kupeleka elimu majumbani mwao pamoja na kuhakikisha hawatupi taka hovyo ili kutunza mazingira pamoja na kuepukana na magonjwa ya milipuko kama Kipundupindu.
Aidha Mradi wa kutoa elimu kwa vitendo juu ya utenganishaji taka Mashuleni unatarajiwa kuzinduliwa rasmi Agosti 30, 2024 katika Shule ya Sekondari Zanaki ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) sambamba na kauli mbiu isemyo “Zingatia utenganishaji taka kwa Utunzaji wa Mazingira”.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.